FPCT Kigoma yatoa msaada kwa watoto yatima
25 June 2024, 11:54
Jamii na wadau wa maendeleo Mkoani Kigoma wameombwa kujitokeza na kuendelea kusaidia watoto yatima wanaolelewa na kituo cha matyazo kilichopo kata ya kalinzi halmashauri ya wilaya kigoma.
Na Lucas Hoha – Kigoma
Kanisa la The Free Pentekosite Church of Tanzania FPCT Mwanga lililopo Manispaa ya Kigoma Ujiji kupitia idara ya Vijana Kanisani wametoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo mafuta, sabuni na sukari vyenye thamani ya zaidi ya shilingi laki tisa katika kituo cha kulea watoto yatima Matyazo kilichopo kata ya kalinzi Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vitu hivyo, katibu wa Kanisa la FPCT Mwanga Mchungaji Amon Anania amesema msaada huo ni sehemu ya wajibu wa kanisa kuihudumia jamii na kutimiza maagizo ya maandiko matakatifu yanayoagiza kuwasaidia watoto yatima.
Kwa upande wake, Mratibu wa idara ya vijana Kanisani Samwel Yusuph Kidaha mbali na kutoa shukrani kwa vijana kuchangia msaada huo ametoa wito kwa mashirika na watu binafsi kujitokeza kutoa msaada kwa watoto hao kwani bado wana mahitaji mbalimbali.
Isac Ngajagu ni Afisa ustawi wa jamii na mlezi wa watoto katika kituo hicho amesema msaada huo ambao umetolewa na kanisa la FPCT Mwanga utasaidia kupunguza baadhi ya gharama kituoni hapo kwani wamekuwa wakitumia zaidi ya shilingi milioni 30 kwa mwezi katika kuwahudumia watoto hao, huku akiongeza kuwa wanatoa msaada kwa watoto waliotelekezwa na wazazi na wale wanaoishi kwenye mazingira hatarishi.
Nao baadhi ya vijana wa Kanisa la FPCT Mwanga wanaeleza sababu iliyowafanya kutoa msaaa huo.
Kituo cha kulea watoto yatima matyazo kwa sasa kina jumla ya watoto 53 na kiko chini ya Kanisani la Anglikana Dayosisi ya Western Tanganyika na kimekuwa kikipokea watoto wenye mahitaji kutoka mikoa mbalimbali Tanzania kwa kushirikiana na serikali.