Tani 3.6 za bidhaa bandia zateketezwa na TBS Kigoma
25 June 2024, 09:55
Jamii mkoani Kigoma imetakiwa kuendelea kushirikiana na wafanyabiashara kubaini na kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na uingizaji wa bidhaa zisizokuwa na ubora kwa mamlaka husika ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Na Emmanuel Matinde -Kigoma
Bidhaa mbalimbali zenye uzito wa tani 3.6 zikiwa na thamani ya shilingi milioni 34 zikiwemo vyakula, vipodozi vyenye viambata vya sumu, nguo za ndani za mitumba na vilainishi vya magari zimeteketezwa mkoani Kigoma na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kutokana na kutokidhi viwango vya ubora.
Afisa Udhibiti Ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania TBS Kanda ya Magharibi Elisha Meshack, amesema bidhaa hizo zimenaswa katika maduka takribani mia moja kote mkoani Kigoma, kufuatia operesheni na kaguzi za kawaida zilizofanywa na TBS kwa kushirikiana na idara zingine za serikali.
Afisa Udhibiti Ubora TBS Kanda ya Magharibi Peter Musiba amesema wataendelea kutumia njia na mbinu mbalimbali kukabiliana na wauzaji wa bidhaa zisizokidhi viwango na zile zilizopigwa marufuku kutumika nchini huku afisa afya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji Roza Aloyce Choma, akitahadharisha juu ya madhara ya kutumia bidhaa hizo.
Baadhi ya wananchi walioshuhudia uteketezaji wa bidhaa hizo uliofanyika katika eneo la Businde Manispaa ya Kigoma Ujiji, walikuwa na haya ya kusema.