Wakuu wa idara acheni kutuma wawakilishi
24 June 2024, 14:56
Serikali wilayani kasulu imetakiwa kuhakikisha wakuu wa idara wanahudhuria mikutano yote na kuacha kutuma wawakilishi kwani wengi wao wamekuwa wakishindwa kujibu hoja ama maswali wanayoulizwa.
Na Hagai Ruyagila – Kasulu
Wakuu wa idara wa halmashauri ya Mji Kasulu wametakiwa kuacha tabia ya kutuma wawakilishi katika vikao mbalimbali vya serikali kutokana na baadhi ya wawakilishi kushindwa kujibu kwa ufasaha baadhi ya hoja.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna jenerali Mstaafu wa jeshi la zimamoto na uokoaji Thobias Andengenye amebainisha hayo katika kikao cha utekelezaji wa mapendekezo ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kwa mwaka 2022/2023 katika ukumbi mkubwa wa mikutano wa halmashauri ya Mji Kasulu.
Andengenye amesema si vizuri wakuu wa idara kutuma wasaidizi wao wakati wakaguzi wanapokuja kukagua idara zao.
Awali akizungumza katika kikao hicho Mkaguzi Mkuu wa nje wa hesabu za serikali mkoani Kigoma Honest Muya amemshauri mkurugenzi wa halmashari ya Mji Kasulu kuwaalika kutembelea miradi ya maendeleo ambayo bado haijakamilika waweze kushauriana endapo kuna changamoto zitatuliwe ili miradi iweze kukamilika kama ilivyo kusudiwa na serikali.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya Mji Kasulu Noel Hanura amesema wamepokea maelekezo yote yaliyotolewa ili kufanikisha mipango ya serikali inafanikiwa huku akiwasisitiza wakuu wote wa idara kuufanyia kazi ushauri huo ili kuondoa changamoto zilizopo.