Joy FM

Watanzania watakiwa kuboresha taarifa zao, daftari la kudumu

19 June 2024, 16:12

Wadau wa uchaguzi wakiwa katika mkutano wa wadau wa uchaguzi wa mkoa wa Kigoma, Kadislaus Ezekiel

Tume huru ya Taifa ya uchaguzi, imewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la wapiga kura ili kurahisisha upatikanaji wa wapiga kura wengi wenye sifa na kurahisisha  upatikanaji wa Viongozi ikiwemo Madiwani, Wabunge na Rais Katika uchaguzi Mkuu hapo Mwakani.

Wananchi mkoani Kigoma wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao wakati wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linalotarajiwa kuzinduliwa mkoani humo tarehe 01 Julai, 2024.

Na Kadislaus Ezekiel – Kigoma

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele wakati akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi wa mkoa wa Kigoma uliofanyika leo tarehe 19 Juni, 2024 katika Halmashauri ya Kigoma Ujiji. 

Jaji Mwambegele amewapongeza wadau wa uchaguzi na wananchi kwa ujumla kwenye mkoa wa Kigoma kwa mkoa wao kuteuliwa kuwa sehemu ya uzinduzi wa uboreshaji huo ambao utafanyika kwenye uwanja wa Kawawa uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB). 

Sauti ya Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele

Ameongeza kuwa Tume ilifikia uamuzi wa kufanya uzinduzi huo kwenye mkoa wa Kigoma baada ya kuzingatia mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa mwamko mkubwa wa wananchi kujitokeza kwenye uboreshaji wa Daftari uliofanyika mwaka 2019/20.

Amesema, uzinduzi wa uboreshaji wa Daftari utatanguliwa na shughuli mbalimbali za uhamasishaji ikiwa ni pamoja na matangazo na tamasha la uborshaji wa Daftari ambalo litafanyika siku ya Ijumaa tarehe 28 Juni, 2024 kwenye uwanja wa Kawawa. 

Wakati akiwasilisha mada, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima, R. K amesema uboreshaji kwa awamu hii ya kwanza utafanyika kwenye mizunguko 13 na kuongeza kwamba baada ya mkoa wa Kigoma uboreshaji utaendelea kwenye mikoa ya Katavi na Tabora.

Mwenyekiti wa tume huru ya taifa ya uchaguzi mheshimiwa, Jaji Jacobs Mwambegele amesema, taratibu zote za uboreshaji wa daftrari la kudumu la wapiga kura zimekamilika, na kuwataka watanzania wenye sifa kujitokeza kwa wingi kuboresha taarifa zao.

Baadhi ya wadau wa uchaguzi mkoani kigoma wakiwa katika mkutano wa uchaguzi, Picha na Kadislaus Ezekiel

Kwa upande wao wadau wa uchaguzi mkoani Kigoma, wameeleza tija ya kuboresha taarifa zao na kwamba ni haki ya kila mtanzania ili kuwa na uhakiki wa kuchagua viongozi bora wanaowataka wenyewe.

Sauti ya wadau wa uchaguzi mkoani Kigoma