Joy FM

Daraja lililokatika kwa elnino lajengwa Tabora

13 June 2024, 08:54

Muonekano wadaraja lilijengwa upya baada ya kukatika kutokana na mvua za Elnino, Picha na Wizara

Serikali imesema itaendelea kuhakikisha miundombinu ya madaraja na barabara iliyoharibika kutokana na mvua za Elnino zilizonyesha msimu wa masika mwaka huu inakarabatiwa ili kurahisisha usafirishaji na kukuza uchumi wa wananchi na jamii kwa ujumla.

Na Tryphone Odace

Wananchi wa Kata ya Kakola na Ikomwa, Manispaa ya Tabora wameishukuru serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kuwafungulia mawasiliano ya daraja katika barabara ya Kakola- Mwibiti.

Daraja hilo liliharibiwa na mvua za Elnino zilizonyesha msimu wa masika mwaka huu.

Wakiongea kwa wakati tofauti Diwani wa Kata ya Kakola Mhe. Chota Lukuiza amesema kuwa kutokana na mvua kubwa za mwaka huu eneo hilo lilikumbwa na mafuriko na kusababisha wananchi wake kushuka kiuchumi.

“Tunamshukuru na kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha za ujenzi wa barabara hii, mvua ya kipindi hiki ilisababisha kukata mawasiliano kwa kata hizi mbili lakini bado ametuletea fedha za dharura na kuweza kujenga ‘Box Kalvati’ na kalvati zingine pamoja na kuinua barabara hii”.

Ameongeza kusema kwamba kutengamaa kwa barabara hiyo inapelekea uchumi wa wananchi wa kata hizo kukua kwani sasa hivi wananchi wanaweza kupita wao wenyewe na kupitisha mazao yao ya biashara.

“Barabara hii ni sehemu kubwa ya uchumi wa wakazi wa kata hizi pia ni kiunganishi cha wilaya ya Uyui na Nzega ambapo hutumika kusafirisha mazao yao ya biashara kutoka mashambani”.

Muonekano wa daraja linalounganisha barabara lililokuwa limekatika na ni kiunganishi cha wilaya ya Uyui na Nzega ambapo hutumika kusafirisha mazao

Naye, Mtendaji wa kijiji cha Ikomwe Bw. Abasi Baluguza amesema wakati wa mafuriko shughuli zao za kiuchumi zilisimama na baadhi ya wananchi ilibidi wazunguke umbali mrefu ili kuweza kufika mjini ambapo ilikuwa gharama kubwa na pia walitumia muda mrefu.

“Kwa kweli jambo ambalo limeshughulikiwa na TARURA, tunamshukuru Mhe. Rais Samia kwa kuliona hili kwani hivi sasa kijiji chetu cha Ikomwe kimefunguka”.

Amesema awali maji yalikuwa mengi sana na wanamshukuru Mungu kwani hakukutokea vifo zaidi ya wananchi kusitisha shughuli zao za kiuchumi, hivyo wanashukuru kwa ujenzi wa ‘Box kalvati’ na barabara hiyo kwa ujumla.

Wakati huo huo Mkazi wa kijiji cha Magowelo Kata ya Kakola Bi. Pili Nasoro amesema kwamba adha kubwa iliwapata wananchi wa vijiji hivyo hususan wajawazito na wanafunzi kutoka vijiji vya karibu ambao hupata huduma katika zahanati na shule za msingi na sekondari zilizopo kata ya Ikomwa.

“Yaani hapa ilikuwa ni bahari, wanafunzi wetu na wajawazito walikuwa wanapata shida, kakini tunamshukuru sana Mama Samia Rais wetu kwa kutuwezesha kurudisha mawasiliano sisi wana Kakola hatuna cha kumlipa kwani sasa tunaweza kwenda kliniki na hata wakulima wanaweza kupeleka bidhaa zao sokoni.

Kaimu Meneja wa TARURA wilaya ya Tabora Mhandisi Gwalugano Mwamwifu amesema kutokana na mvua za mwaka huu barabara nyingi ziliathiriwa na mvua hizo na moja ya maeneo waliyorudisha mawasiliano ni barabara hiyo ya Kakola-Mwibiti ambapo wameweza kurudisha mawasiliano kwa 100%.

Amesema kazi iliyofanyika ni ujenzi wa ‘Box Kalvati’ yenye urefu wa mita 10, Kalvati laini 5, kuchimba mitaro Km. 3 kwaajili ya kupeleka maji kwenye kalvati pamoja na kuinua tuta la barabara lenye urefu wa Km. 7 ambayo iliathiriwa na mvua.