Joy FM

Wahandisi washauri watakiwa kusimamia miradi kwa ukaribu

11 June 2024, 08:56

Naibu katibu mkuu anayesimamia miundombinu Mhandisi Rogatus Mativila, Picha na Wizara

Serikali imesema haitawavumilia wahandisi washauri wanaoshindwa kusimamia vyema miradi mbambali ya barabara inayotekelezwa maeneo mbalimbali nchini.

Na Tryphone Odace

Naibu Katibu Mkuu anayesimamia miundombinu OR-TAMISEMI Mhandisi Rogatus Mativila amewataka Wahandisi Washauri wanaosimamia miradi mbalimbali ya miundombinu ya barabara nchini kusimamia kwa ukaribu miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati.

Mhandisi Mativila ameyasema hayo leo tarehe 10 Juni,2024 wakati akikagua ujenzi wa jengo la ofisi la wahandisi katika manispaa ya Tabora ambalo lipo chini ya mradi wa TACTIC unaosimamiwa na TARURA.

Naibu Katibu Mkuu anayesimamia miundombinu OR-TAMISEMI Mhandisi Rogatus Mativila, Picha na Wizara

“Mhe. Rais Dkt. samia Suluhu Hassan anahangaika kutafuta fedha ili kuhakikisha wananchi wanapata barabara,wataalam lazima mbadilike na kusimamia kwa ukaribu ujenzi wa miradi hii.
Mkandarasi huyu angekuwa anasimamiwa kwa ukaribu angeshakuwa amemaliza hapa”.

Hata hivyo Mhandisi Mativila amewataka wataalam hao kuhakikisha wanasimamia ubora wa ujenzi ili wakandarasi wakamilishe kazi kwa wakati.

Aidha, amemtaka Mhandisi Mshauri UNITEC Civil Consultants ltd kuhakikisha anasimamia kwa karibu ujenzi huo na ifikapo mwezi Agosti mwaka huu jengo hilo liwe limekamilika.

Naibu Katibu Mkuu anayesimamia miundombinu OR-TAMISEMI Mhandisi Rogatus Mativila, Picha na Wizara

Ujenzi wa jengo la ofisi la wahandisi linalogharimu takriban milioni 800 lilianza ujenzi wake Novemba 2023 na lilitarajiwa kukamilika 15 Juni,2024 na kuagiza ujenzi huo uwe umekamilika ifikapo Agosti 2024 na linajengwa na mkandarasi CICO Contractor.