Joy FM

“Wafanyabiashara fanyeni miamala benki kuepuka fedha bandia”

5 June 2024, 12:12

Washiriki wa mafunzo yanayotolewa na BOT wakiangalia kwenye taa maalumu pesa bandia na halali inavyoonekana na alama zake, Picha na BoT

Wafanyabiashara nchini wametakiwa kutumia benki kuu ya tanzania ili kuhakiki pesa zao kabla ya kufanya miamla ya pesa kwa lengo la kuepuka kuoewa pesa bandia.

Na Tryphone Odace

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa wito kwa wafanyabiashara nchini kufanya miamala ya kifedha benki ili kuepuka kupewa fedha bandia ambazo zinatengenezwa na kusambazwa na watu wenye nia mbaya kwa taifa.

Hayo yamebainishwa na Meneja Uendeshaji wa BoT Tawi la Dodoma, Bw. Nolasco Maluli, wakati akifundisha juu ya alama za usalama za noti zetu kutofautisha na pesa bandia kwa waandishi wa habari katika ukumbi wa jengo la BoT jijini Dodoma.

Amesema kuwa pesa bandia inakuwa haina alama muhimu ambazo zinatakiwa kuwepo kwenye pesa halapo ambapo baadhi ya alama za usalama huonekana kwa macho na nyingine kwa kutumia vifaa maalumu vinavyopatikana katika maeneo ya benki ili viweze kuwasaidia wananchi kutambua pesa hizo.

Meneja uendeshaji Benki kuu ya tanzania Tawi la Dodoma Nolasco Maluli akielekeza namna ya kufahamu pesa bandia, Picha na BoT

Aidha, amesema kuwa endapo mtu atakamatwa na pesa bandia kwa mujibu wa sheria anaweza kupata kifungo jela. Amesema wamekuwa wakikamata watu wenye pesa bandia na sheria kufuata mkondo wake.

Hata hivyo, ameendelea kuwasisitiza wafanyabiashara kuwa na taa maalumu za utambuzi wa pesa hizo lakini pale wanapotilia shaka na hawana uwezo wa kupata taa maalumu basi waende na wateja wao benki na malipo yafanyikie hapo ili kuepuka kupata pesa bandia.

“Baadhi ya wafanyabiashara hasa wa mazao huko vijijini hawaelewi kuhusu fedha bandia hali inayosababishia kujikuta natatizoni, kwani sisi ni yule anayekamatwa na pesa bandia ndiye mtuhumiwa. Kwa hiyo, endapo huwezi kutambua noti halali, nenda benki, pale kuna vifaa maalumu pesa zitaangaliwa na ikiwa ni pesa halali utachukua pesa zako na kama sio halali mteja wako atakamatwa ili sheria ifuate mkondo wake,” amesema hayo Bw. Maluli.

Katika hatua nyingine amesisitiza wananchi kupenda kufanya miamala kidigitali na kutunza pesa benki ili kupunguza uwepo wa pesa bandia na matumizi yake.

Washirika wa mafunzo ya BoT wakiwa katika mafunzo ya kutambua pesa bandia, Picha na BoT