Joy FM

BoT yawataka wananchi kutunza fedha kwa njia sahihi

5 June 2024, 11:43

Meneja Msaidizi Sarafu kutoka Benki Kuu Tawi la Dodoma, Matilda Luvinga, BoT

Katika kuhakikisha fedha zilizopo kwenye mzunguko nchini zinaendelea bora na kutokuwa na madhara kwa watumiaji, Benki kuu ya tanzania imeelekeza wananchi kuhakikisha wanaweka pesa zao katika mazingira rafiki.

Na Tryphone Odace

Wito umetolewa kwa wananchi nchini kutunza fedha kwa njia sahihi ili kuepuka kupata magonjwa na kuliongezea taifa hasara kutokana na uharibifu wa fedha.

Hayo yamebainishwa na Meneja Msaidizi Sarafu kutoka Benki Kuu Tawi la Dodoma, Matilda Luvinga wakati akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka mikoa saba ya Tanzania chini ya Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) katika jengo la Benki Kuu ya Tanzania jijini Dodoma.

Amesema kuwa wananchi wamekuwa wakitunza fedha kwa njia ambazo sio nzuri na kupelekea pesa kuharibika kwa haraka na kuisababishia nchi hasara katika kutengeneza pesa mpya zitakazotumiwa.

Waandishi wa habari kutoka klabu za waandishi wahabari kutoka mikoa mbalimbali nchini wakiwa kwenye mafunzo yaliyoandaliwa na Benki kuu ya Tanzania, Picha na BOT

“Kumekuwa na tabia ya watu kutupa pesa chini kwenye harusi au sherehe mbali mbali wengine wanachorachora pesa, wengine mnatunza pesa kwenye sehemu za siri, kwenye matiti, kwenye soksi na wengine kuzikunjakunja. Ni kosa la kisheria na ni jinai kwani mamlaka pekee iliyo na wajibu wa kuharibu pesa kutokana na vigezo vilivyowekwa,” amesema Bi. Luvinga.

Aidha, amesema kuwa kuna onyo lilitoka mwaka 2002 likielekeza namna ya kutunza pesa vizuri na mwaka 2021 ulitoka waraka wa kuchukua hatua kwa yoyote anaechezea pesa na kusabbisha pesa kuharibika kwa haraka na kupelekea kupata magonjwa hasa pesa inapotunzwa kwenye matiti na kusababisha wanawake kupata magonjwa kama vile saratani hali ambayo inapunguza vipato vya familia kwa matibabu.

Aidha, amesema Serikali inatumia pesa nyingi katika kutengeneza pesa hizo hivyo kusababisha kushindwa kupata maendeleo ya kiuchumi kama kuongezwa kwa shule, vituo vya afya na miundombinu mingine yenye kuleta manufaa kwa wananchi.

Bi. Luvinga amesema kuwa wananchi hasa wafanyabiashara hawana budi kupata mapochi katika biashara zao ambazo zitawasaidia kutunza kirahisi pesa zao na kusalia salama ili pesa iendelee kuwa nzuri na kusaidia katika kukuza uchumi wa nchi yetu katika kuongeza miundombinu hitajika kwa wananchi na kuepuka hasara ya kurudia utengenezaji wa pesa nyingine huku akisisitiza kuwa pesa ni tunu ya Taifa hivyo ni takwa la kisheria iweze kulindwa.

Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya 2006 kifungu cha 26 inatoa mamlaka kwa Benki Kuu ya Tanzania pekee katika kuweza kusanifu na kutengeneza pesa ya Tanzania, hivyo ni kosa la jinai kwaa yoyote atakaebainika anaharibu au anatunza pesa vibaya.