Joy FM

Mwenyekiti wa mtaa matatani kwa kuuza eneo la shule Kigoma

13 Aprili 2026, 16:46

Muonekano wa eneo la shule lililouzwa kwa mtu, Picha na Sadik Kibwana

Viongozi wa serikali za mitaa wilayani Kigoma wametakiwa kuacha kuhusika katika migogoro ya ardhi kati ya Wananchi, viongozi na maeneo ya serikali.

Na Sadick Kibwana

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Rashid Chuachua, amemsimamisha uongozi Mwenyekiti wa Mtaa wa Mgeo, Azizi Ibrahim, na kuagiza akamatwe kwa tuhuma za kuingilia na kuuza eneo la Shule ya Msingi Mgeo katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Dk. Chuachua alitoa maagizo hayo baada ya kutembelea eneo la shule kufuatia taarifa za uvamizi na uuzwaji wa eneo hilo, ambapo alieleza kuwa maelekezo ya kusimamisha ujenzi yalipuuzwa.

Onyo hili limetolewa ili kuhakikisha kuwa viongozi hao wanatekeleza majukumu yao kwa haki na kusaidia kutafuta suluhisho la kudumu badala ya kuwa chanzo cha migogoro hiyo kama anavyoeleza Mkuu wa Wilaya Kigoma Dkt Rashid ChuaChua kufuatia kuuzwa sehemu ya eneo la shule ya Msingi Mgeo ambalo linaelezwa kuuzwa na Mwenyekiti wa mtaa huo.

Hata hivyo,  Aliyekuwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Mgeo Kata ya Buhanda Azizi Ibrahim amesema eneo hilo limeuzwa likiwa nje ya eneo la shule hiyo ya msingi.

Muonekano wa eneo la shule lililouzwa kwa mtu, Picha na Sadik Kibwana

Aidha, Mpima Ardhi Manispaa Halima Mbaga amesema nyumba hiyo imechukua sehemu kidogo ya shule na sehemu nyingine ni barabara.

Kutokana na changamoto hiyo Dkt. Chua Chua amemuondoa kwenye nafasi ya  Uwenyekiti Mwenyekiti wa Mtaa huo kupisha uchunguzi na kuelekeza vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina zaid.

Hatua hii inalenga kuimarisha utawala bora na uwajibikaji kwa viongozi, hasa katika maeneo yenye changamoto za ardhi na kupunguza kadhia hiyo.

Awali, Afisa Mtendaji wa Kata ya Buhanda, Zeenat Ambikai, alisema nyaraka zinaonyesha eneo hilo liliuzwa mwaka 2021, lakini ujenzi ulianza Januari mwaka huu, licha ya shule hiyo kuanzishwa tangu mwaka 2006.