Joy FM
Joy FM
13 Aprili 2026, 15:16

Shirika la World Vision kupitia mradi wa Kasanda limetoa zawadi kwa watoto wa Kata ya Mugunzu wilayani Kakonko mkoani Kigoma zenye thamani ya shilingi milioni 52.2 ambapo misaada iliyotolewa inalenga kuendelea kuwafanya watoto hao kuwa wenye tabasam katika masomo yao.
Na Mwandishi Wetu
Shirika la World Vision limeadhimisha siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa watoto walioandikishwa katika mradi wa Kasanda kwa kufanya hafla maalum inayolenga kuimarisha ustawi na furaha ya watoto katika jamii ambapo Hafla hiyo imewakutanisha watoto, wazazi na wadau mbalimbali katika jamii.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika Jumamosi Aprili 11, 2026 Katika Kata ya Mugunzu, Mgeni Rasmi Majaliwa Tryphone, amewataka wazazi kuwaelezea umuhimu wa malezi bora na kuwa karibu kwa watoto, huku akieleza kuwa msingi wa makuzi mema huanzia nyumbani.

Aidha ameendelea kuitaka jamii kushirikiana kwa pamoja katika kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa kuwapa elimu, kuwasikiliza na kujenga mahusiano ya karibu yatakayosaidia watoto kuwa huru kueleza changamoto zao.
Hata hivyo amepongeza juhudi za shirika hilo kwa kuendelea kusaidia watoto na familia zao, akisema kuwa mchango huo unaimarisha ustawi wa watoto na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mratibu wa Mradi wa Kasanda Innocent Innocent Juvenary, amesema maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuwapa watoto furaha, kuwajengea kujiamini na kuhamasisha jamii kuthamini haki za mtoto.
Aidha amesema kuwa maadhimisho hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha mshikamano wa kijamii na kulinda haki za watoto katika jamii ambapo ameeleza kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na jamii katika kuhakikisha watoto wanapata malezi bora, ulinzi na stahiki za maendeleo ili kufikia ndoto zao.
Baadhi ya Wazazi na walezi walioshiriki hafla hiyo wamelishukuru shirika la World vision kwa kuendelea kuwa karibu na watoto wao huku wakisema maadhimisho hayo yanachangia kwa kiasi kikubwa kujenga kujiamini na furaha kwa watoto.