Joy FM

Wananchi wafurika kambi ya madaktari Kigoma

6 April 2026, 11:38

Mkuu wa Mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro akiwa amewasili katika uwanja wa kambi ya madaktari bingwa, Picha na Mwandishi wetu

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amezindua kambi ya matibabu ya macho bila malipo, inayoendelea katika Kituo Cha Kiislam cha Alhulbayt-Ujiji, Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Na Mwandishi Wetu,

Wananchi zaidi ya watu 1500 kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa Kigoma wamejitokeza katika siku ya kwanza kati ya siku nne za kambi ya matibabu ya Kibingwa ya Macho inayofanyika mjini Kigoma huju wakieleza kuwa kambi hizo ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa kipato cha chini.

Wakizungumza katika kambi hiyo ya matibabu chini ya uratibu wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Lalji Foundation wananchi hao wamesema kuwa kambi hizo zinasaidia kusogeza karibu huduma za matibabu za kibingwa lakini pia kupunguza gharama kwa wananchi.

Mkuu wa Mkoa akiwa katika kambi ya madaktari, Picha na Mwandishi wetu

Mmoja wa wananchi waliohudhuria matibabu kwenye kambi hiyo,Seleman Saidi wa Ujiji Kigoma alisema kuwa huduma za kibingwa za macho hazipatikani mkoani Kigoma hivyo kuwepo kwa kambi hiyo kunaweza watu wengi kupata huduma hiyo.

Akizungumza kuhusu kambi hiyo ya madaktari Mlezi wa Taasisi ya Lalji Foundation, Mohsin Abdallah alisema kuwa katika siku ya kwanza ya kambi hiyo idadi kubwa ya watu walikuwa wamejitokeza wakitarajia watu 6000 kupata huduma hiyo kwa siku nne.

Abdallah alisema kuwa katika kambi hiyo jumla ya madaktari bingwa, wahudumu wa afya na wataalam mbalimbali 28 kutoka jijini Dar es Salaam watatoa huduma kwenye kambi hiyo huku madaktari bingwa na wahudumu na wataalam 10 kutoka Hospitaali ya mkoa Kigoma maweni watasaidia katika utoaji huduma ambapo watu na operesheni Zaidi ya 500 za macho zitafanyika.

Mama akipatiwa matibabu ya macho mbele ya mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Picha na Mwandishi wetu

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa Kigoma, Balozi Simon akizungumza wakati akizindua kambi hiyo alisema kuwa kambi hizo za matibabu ya Kibingwa zimekuwa na msaada mkubwa kwa serikali katika kusaidia kusogeza huduma kwa wananchi lakini pia kusaidia wananchi wasio na uwezo kupata huduma hizo bila malipo.

Mkuu wa Mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro akizungumza na wananchi waliojitokeza kupata matibabu ya macho, Picha na Mwandishi wet