Joy FM
Joy FM
31 March 2026, 10:56

Amani na upendo huimarisha mshikamano wa kijamii na wat wanapoishi kwa kuheshimiana na kusaidiana, hujenga umoja unaowezesha jamii kuishi kwa utulivu bila migogoro.
Na Hagai Ruyagila
Wakristo Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma wamehimizwa kuendelea kuishi maisha ya kudumisha amani, upendo na mshikamano popote watakapokuwepo ili kuimarisha amani katika taifa.
Wito huo umetolewa na Mchungaji Kiongozi Gidion Kaleke wa Kanisa la Anglikana Mchungaji Mwema, lililopo Halmashauri ya Mji Kasulu, wakati wa ibada takatifu ya Jumapili iliyofanyika Machi 29 mwaka huu
Mchungaji Kaleke, amesema kuwa amani ni msingi muhimu wa maendeleo, akibainisha kuwa familia au taifa lenye amani hupata fursa ya kupiga hatua kiuchumi na kijamii, huku akionya kuwa kukosekana kwa amani kunakwamisha maendeleo.

Aidha, Mch, Kaleke amewasihi waumini kumtolea Mungu sadaka ya shukrani wanapoelekea Sikukuu ya Kufufuka kwa Yesu Kristo (Pasaka), akieleza kuwa kufanya hivyo ni sawa na kupanda mbegu itakayowaletea mafanikio katika nyanja mbalimbali ikiwemo afya, elimu na maisha ya kila siku.
Kwa upande wao, baadhi ya waumini wa Kanisa la Anglikana Mchungaji Mwema wamesema mafundisho hayo yamewajenga kiimani na kuwapa hamasa ya kuishi kwa amani pamoja na kushiriki kikamilifu katika matendo ya imani kuelekea sikukuu ya Pasaka.