Joy FM
Joy FM
27 March 2026, 18:10

Serikali imeendelea kuwawezesha vijana kupitia mikopo ya asilimia kumi, huku waendesha bodaboda katika Kata ya Makere wilayani Kasulu mkoani Kigoma wakisema hatua hiyo imebadili maisha yao kwa kiasi kikubwa.
Na Mwandishi wetu
Umoja wa maafisa usafirishaji maarufu kama bodaboda katika Kijiji na Kata ya Makere, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma, wameipongeza Serikali kwa kuwawezesha kupata mikopo ya asilimia kumi, hatua iliyowawezesha kununua pikipiki na kuboresha maisha yao kiuchumi.
Zaidi ya waendesha bodaboda ishirini wameungana na kuanzisha kikundi cha usafirishaji, jambo ambalo limewasaidia kujikwamua kiuchumi, kupunguza utegemezi, na kuwapatia ajira vijana waliokuwa wakikaa mitaani bila shughuli za kufanya.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Makere, Sixmundi Kato, amesema kuwa hadi sasa vijana wamepatiwa mikopo inayozidi shilingi milioni 130, hali iliyochangia kupungua kwa matukio ya uhalifu na kuwahamasisha vijana kujikita katika shughuli halali za kujipatia kipato.

Hata hivyo, wito umetolewa kwa vijana kuendelea kuungana na kusajili vikundi vyao kisheria ili waweze kunufaika na mikopo hiyo, huku Serikali ikiendelea kutoa mafunzo ya kuwawezesha katika shughuli za uzalishaji mali.