Joy FM
Joy FM
26 March 2026, 16:36

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua leo Machi 25, 2026 ameanza Kliniki ya kutatua migogoro ya ardhi kwa Wananchi wenye matatizo ya ardhi Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Wlaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua, ameanza awamu ya pili ya kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero za ardhi kwa wakazi wa wilaya hiyo kufuatia Samia Ardhi Kliniki, iliyomalizika wiki kadhaa zilizopita.
Katika awamu hii ya pili Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua, ameanza kusikiliza kero za ardhi kwa wakazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji katika Uwanja wa Mwanga Communty Center ambapo wananchi wametoa kero zao.

Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa siku ya kwanza ya kusikiliza kero zinazohusiana na masuala ya ardhi, Dkt. Chuachua, amewasihi wananchi wenye kero za ardhi waendelee kujitokeza na kueleza kero zao ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.
Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, wamesema kuwa kliniki za ardhi zimesaidia kutatua changamoto za masuala ya ardhi ikiwemo umiliki pamoja na fidia kwa maeneo ambayo yamechukuliwa na serikali kwa ajili ya kujenga miundombinu ya huduma za kijamii.

Kwa upande wake, Afisa Ardhi Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Kigoma, Elias Mwazembe, amesema awamu hii ya pili ya kliniki ya ardhi inalenga kumaliza migogoro iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma pamoja na Manispaa ya Kigoma Ujiji.