Joy FM
Joy FM
25 March 2026, 15:58

Wananchi wa Mtaa wa Kanazi Kata ya Ruhita Halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi katika kuimarisha ulinzi shirikishi, ili kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao unaendelea kudumishwa.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Polisi Jamii wilaya ya Kasulu, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Inspector Willy Lupa, wakati akitoa elimu ya ulinzi na usalama kwa wananchi wa mtaa wa Kanazi.
Inspector Lupa amesema kuwa hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana endapo usalama utakuwa dhaifu, huku akieleza kuwa sababu ya kuanzishwa kwa vikundi vya ulinzi shirikishi ni kuimarisha ulinzi, usalama na kudumisha amani katika jamii.

Aidha, amesisitiza kuwa vikundi hivyo vya ulinzi shirikishi vinapaswa kuwa na wanachama waaminifu, kwani uwepo wa watu wasio waadilifu unaweza kuchangia kuendelea kwa vitendo vya uhalifu badala ya kuupunguza.
Pia Inspector Willy Lupa amewataka wananchi kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali au vyombo vya ulinzi na usalama pindi wanapoona viashiria au matukio ya uhalifu, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Kanazi wamekiri kuwepo kwa vitendo vya wizi katika maeneo yao, huku wakiomba serikali kuendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika, ili iwe fundisho kwa jamii nzima.