Joy FM

Wakulima andiko la miradi ya kilimo wapewa mashine 48 Kasulu

25 March 2026, 11:56

Vifaa na mashine zilizotokewa kwa washindi wa andiko Bora la Mradi wa kilimo, Picha na Hagai Ruyagila

Mradi wa Kilimo Tija Kigoma (KITIKI) umekabidhi mashine na vifaa 48 kwa washindi wa andiko bora la kilimo biashara kutoka wilaya za Kasulu, Kibondo na Kakonko mkoani Kigoma.

Na Hagai Ruyagial

Mashirika ya World Vision Tanzania na Good Neighbors kupitia mradi wa Kilimo Tija Kigoma (KITIKI), unaofadhiliwa na Serikali Korea Kusini kupitia Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), wamekabidhi mashine na vifaa 48 kwa washindi wa andiko bora la miradi ya kilimo biashara kutoka wilaya za Kasulu, Kibondo na Kakonko ili kuwasaidia kuboresha shughuli za kilimo.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Mwakilishi wa Meneja wa Kanda wa Mradi wa KITIKI kutoka World Vision Tanzania, Eric Kidohera amesema lengo la mpango huo ni kuendeleza mawazo ya wakulima ili kuwasaidia kutoka katika kilimo cha mazoea na kujikita katika kilimo chenye tija.

Sauti ya Mwakilishi wa Meneja wa Kanda wa Mradi wa KITIKI kutoka World Vision Tanzania, Eric Kidohera

Mkuu wa wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu, amewapongeza wadau wote waliofanikisha upatikanaji wa vifaa hivyo, huku akiwataka wakulima waliopokea zawadi hizo kuvithamini na kuvitunza ili viweze kuleta manufaa kipitia sekta ya Kilimo.

Sauti ya Mkuu wa wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu, Picha na Hagai Ruyagila

Meneja wa Mradi kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Wilayani Kasulu Heshima amesema kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha sekta ya kilimo kwa wakulima wa eneo hilo.

Sauti ya Meneja wa Mradi kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP)
Vifaa na mashine zilizotokewa kwa washindi wa andiko Bora la Mradi wa kilimo Biashara kutoka wilaya za Kasulu, Kibondo na Kakonko, Picha na Hagai Ruyagila

Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Uchumi na Uzalishaji kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma James Peter amesema wazo la KITIKI ni wazo linalokwenda kuunga mkono mikakati ya Serikali ya Tanzania katika kuendeleza sekta ya kilimo, ikiwemo kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji na kipato.

Sauti ya Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Uchumi na Uzalishaji kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma James Peter
Katibu tawala msaidizi anayeshughulikia uchumi na uzalishaji kutoka ofisi ya Mkuu wa mkoa wa kigoma James Peter, Picha na Hagai Ruyagila

Baadhi ya wakulima walionufaika na mradi huo wamewashukuru wadau wa maendeleo kwa kuwapatia vifaa hivyo, ikiwemo jenereta, mashine za umwagiliaji, wakisema vitawarahisishia shughuli za kilimo ambazo hapo awali zilikuwa na changamoto kubwa.

Sauti ya Baadhi ya wakulima
Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu ,viongozi mbalimbali na wakulima katika picha ya pamoja, Picha na Hagai Ruyagila

Mashine na Vifaa vilivyotolewa ni jenereta, mashine za umwagiliaji, mashine za kupukuchulia mahindi, mashine za kupandia na kuwekea mbolea, mashine za kusukuma maji, powertiller, mashine za kupalilia, mashine za kushonea magunia, mipira kwa ajili ya umwagiliaji na mashine za kupulizia viuatilifu za injini ya mafuta.