Joy FM
Joy FM
21 March 2026, 15:21

Upandaji miti ni jambo muhimu katika maisha ya binadamu na viumbe wengine duniani na miti imekuwa na mchango mkubwa katika kuhifadhi mazingira, kuboresha hali ya hewa, na kusaidia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Evance Mallasa, amewahimiza wananchi kuendelea kupanda na kutunza miti rafiki ya mazingira kwa wingi kwenye maeneo yao ili kulinda mazingira na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Bukirilo Kata ya Gwanumpu, Mallasa alisema misitu ni rasilimali muhimu kwa ustawi wa dunia na maendeleo ya kiuchumi.
“Misitu ina mchango mkubwa katika utunzaji wa mazingira na pia ni chanzo cha kipato, hivyo ni muhimu kupanda miti kwa wingi,” alisisitiza Kanali Malassa.

Askari mhifadhi misitu kutoka TFS, Winfrida Chacha ameeleza kuwa katika maadhimisho hayo, jumla ya miche ya miti 1,000 imepandwa katika Kijiji cha Bukirilo huku miche mingine zaidi ya 290,000 ikiwa imepandwa katika Vijiji mbalimbali katika Wilaya ya Kakonko kama sehemu ya juhudi za wilaya i ya mazingira.
Kwa upande wake, mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bukirilo Boniphace Charles Mlyakado, aliwahimiza wanafunzi kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa miti iliyopandwa ili kuhakikisha inakua na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.
“Kwa miti hii iliyo pandwa hapa sisi kama shule na walimu kushirikiana na wanafunzi tutahakikisha inatunzwa kwa umakini ili iweze kukua” alisema mwalimu Mkuu.

Naye mwenyekiti wa kijiji cha Bukirilo Renatus Didiye, alisisitiza ushirikiano wa wananchi katika kulinda miti hiyo, akieleza kuwa mafanikio ya juhudi hizo yanategemea uwajibikaji wa kila mmoja.
Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani hufanyika machi 19 kila mwaka, yakilenga kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa misitu na uhifadhi wa mazingira.