Joy FM

TAKUKURU Kigoma yatoa Iftar kujumuika na jamii

18 March 2026, 14:48

Viongozi na wadau wakishiriki katika iftar iliyoandaliwa na TAKUKURU Kigoma, Picha na Mwandishi wetu

Vitendo vya ukatili ambavyo vimeendelea kutokea katika jamii viongozi wa dini wamehimizwa kuendelea kutoa elimu ili kusaidia kudhibiti vitendo hivyo

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua, ametoa wito kwa viongozi na waumini wa dini ya kiislam na wananchi kwa ujumla kutumia mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kutafakari kuhusu namna wanavyoweza kuendelea kudumisha upendo, mshikamano, amani na utulivu kuanzia ngazi ya familia mpaka ngazi ya Taifa.

Ametoa wito huo kwenye Iftar iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoa wa Kigoma, ambapo viongozi mbali mbali akiwemo Sheikh Mkuu  wa Mkoa wa Kigoma, Sheikh Hassan Kiburwa pamoja na waumini wa dini ya kiislam wameshiriki Iftar hiyo.

Mkuu wa Wilaya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua, Picha na Mwandishi wetu

Dkt. Chuachua, amesema hayo kufuatia kukithiri kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto katika maeneo kadhaa ya wilaya ya Kigoma, yakiwemo matukio ya hivi karibuni yaliyotokea kata za Katubuka na Kibirizi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, ambapo Mkuu huyo wa Wilaya ya Kigoma amesisitiza ulinzi kwa watoto.

Aidha Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua, ametoa wito kwa wananchi wilayani humo  kuwatumia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoa wa Kigoma kama rafiki ili kufichua matendo mbali mbali yanayoashiria rushwa.

Akizungumza wakati wa Iftar hiyo Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Sheikh Hassan Idd Kiburwa, ameishukuru TAKUKURU kwa kuandaa Iftar hiyo, lakini akatumia nafasi hiyo kuwaomba waislam kuyachukua mema yote waliyoyaishi katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kuyaendeleza katika miezi mingine inayofuata ili kuendelea kuwa watu wazuri.

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Sheikh Hassan Idd Kiburwa, Picha na Mwandishi wetu

Kwa upande wake Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Kigoma, John Mgallah, amesema kupitia huduma ya TAKUKURU RAFIKI, wameendelea kushirikiana na wadau mbali mbali kujua changamoto zilizopo na kuzipatia ufumbuzi.

Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Kigoma, John Mgallah, Picha na Mwandishi wetu