Joy FM

Wananchi Kasulu wanufaika na Miche 120,000 ya Kahawa Bure

9 March 2026, 21:00

Wakazi wa Kijiji cha Bugaga na maeneo ya jirani katika Wilaya ya Kasulu wakiwa wamekusanyika ili kupokea miche 120,000 ya kahawa aina ya Arabica iliyotolewa bure. Picha Emmanuel Kamangu

Wakazi wa Kijiji cha Bugaga na maeneo ya jirani katika Wilaya ya Kasulu wamejitokeza kwa wingi kupokea miche 120,000 ya kahawa aina ya Arabica iliyotolewa bure na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu katika awamu ya pili ya ugawaji. Hatua hiyo inalenga kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa pamoja na kuimarisha uchumi wa wakulima wa eneo hilo.

Akizungumza wakati wa zoezi la ugawaji wa miche hiyo kijijini Bugaga, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Wakili Emmanuel Ladislaus, amesema mpango huo unaonesha dhamira ya serikali ya kuwasaidia wananchi kuboresha uchumi wao kupitia kilimo.

Amesema serikali inaendelea kutoa fursa mbalimbali kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara na kuwataka wananchi waliopokea miche hiyo kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya kuiuza.

“Serikali inawajali wananchi wake ndiyo maana inaendelea kutoa fursa hizi muhimu. Tunawaomba wakulima wasiifanyie biashara miche hii. Tutakapobaini mtu anaiuza, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” amesema Wakili Ladislaus.

Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Mikidadi Mbaruku, amesema hadi sasa jumla ya miche 420,000 ya kahawa tayari imeshasambazwa katika maeneo mbalimbali ya halmashauri hiyo.

Ameongeza kuwa wataalamu wa kilimo wataendelea kuwapatia wakulima elimu ya namna bora ya kupanda na kuitunza miche hiyo ili kuongeza tija mashambani, bila kuwatoza gharama yoyote.

Baadhi ya wananchi waliopokea miche hiyo wameishukuru serikali kwa kuwapatia miche ya kahawa bure, wakisema hatua hiyo itawasaidia kuimarisha kipato chao kwa kuanza kulima zao la kudumu.

Mmoja wa wananchi hao, Peter Bisakala, amesema mpango huo utawasaidia wakulima wengi kuanza kilimo cha kahawa badala ya kutegemea mazao ya muda mfupi ambayo mara nyingi hayatoi faida ya kudumu.

Naye Mariam Masoud amesema ugawaji wa miche hiyo ni msaada mkubwa kwa wananchi kwani utawawezesha kuanzisha kilimo cha zao la kudumu kitakachochangia kuboresha kipato cha familia zao na kuinua hali ya maisha kwa ujumla.