Joy FM

Wanawake waaswa kuwekeza ili kujikwamua kiuchumi Kigoma

9 March 2026, 07:59

Mkuu wa Wilaya Uvinza Mh. Dinah Mathamani akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake, Picha na Ofisi ya Mawasiliano Kigoma

Jamii mkoani Kigoma imetakiwa kutoa taarifa kwa wakati  kuhusu vitendo vya ukatili vinavyotendeka dhidi ya wanawake na watoto ili kudumisha ulinzi na usalama kwa makundi hayo.

Na Mwandishi wetu

Wanawake mkoani Kigoma wamehimizwa kuendelea kutumia fursa zilizopo kuwekeza katika shughuli za kiuchumi pamoja na kujitokeza kushika nafasi mbalimbali za uongozi ili kuongeza mchango wao katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mh.Dinah Mathamani, alipokuwa akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Wilaya ya Kakonko kwenye viwanja vya Ofisi ya Kata ya Kasanda.

Wanawake wakicheza wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake, Picha na Mwandishi wetu

Mh.Dinah amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mazingira rafiki yanayowawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, uchumi na uongozi kupitia sera, programu na fursa mbalimbali za uwezeshaji.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya Uvinza

Amesisitiza kuwa wanawake wanapaswa kuzitumia kikamilifu fursa hizo kwa kujiingiza katika shughuli za uzalishaji, biashara, kilimo cha kisasa pamoja na kujiunga katika vikundi vya kiuchumi ili kujiongezea kipato na kujikwamua kiuchumi. Pia amewahimiza wanawake kujitokeza kugombea na kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika jamii ili sauti zao zisikike katika maamuzi ya maendeleo.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa, amesema serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo inayolenga kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuhakikisha wanapata fursa sawa katika uongozi, maamuzi na ushiriki wa maendeleo ya Taifa.

Sauti Katibu tawala mkoa wa Kigoma
Katibu tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa, Picha na Mwandishi wetu

Aidha, amewahimiza wanawake kuwa wabunifu, kujiamini na kutumia maarifa waliyonayo ili kunufaika na fursa za mikopo, mafunzo ya ujasiriamali pamoja na nafasi za uongozi zinazopatikana katika jamii.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 8 Machi yakilenga kuhamasisha usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake na kutambua mchango wao katika maendeleo ya jamii.