Joy FM

Mradi wa KITIKI ulivyosaidia wakulima kuongeza uzalishaji Kibondo

5 March 2026, 09:31

Wakulima wakiwa wanafurahia mahindi yaliyovunwa ikiwa ni matokeo ya mradi wa KITIKI, Picha na mtandao

Wakulima wameiomba serikali na wadau wengine kuendelea kutoa elimu ya upimaji wa udongo ili kutambua aina za viuatilifu vya kutumia kulingana na aina ya udongo

Na Mwandishi wetu

Baadhi ya wakulima katika kijiji cha Mukarazi kata ya Mabamba Wilayani Kibondo Mkoani Kigoma wamesema mradi wa Kilimo Tija Kigoma KITIKI umewasaidia katika upatikanaji wa pembejeo za kilimo kupitia vikundi na kuongeza uzalishaji baada ya kupata elimu ya kilimo chenye tija.

Mradi huo wa KITIKI unafadhiliwa na serikali ya Korea Kusini kupitia Shirika la Maendeleo la Korea kusini (KOICA) na msimamizi ni Shirika la Maendeleo ya Chakula Duniani WFP na utekelezaji unasimamiwa na Shirika la World Vision Tanzania ambao wanasimamia uzalishaji, usimamizi wa mazao na kuweka akiba katika kilimo pamoja na Shirika la Good Neighbours ambao wao wanasimamia masoko na kuongeza manufaa.

Tangu mwaka 2023 yapo manufaa ambayo yamepatika ambapo Bw. Samson Katabila aliyemwakilisha Meneja mradi mkoa wa Kigoma katika kuadhimisha siku ya mkulima kwenye kijiji cha Mukarazi amesema kikundi cha Tujikwamue Mukarazi kimekuwa kikifanya vizuri kutokana na elimu ambayo wametoa ya kilimo.

Amesema awali changamoto ilikuwa ni mitaji kwa wakulima, ndipo mradi ukaanzisha mbinu ya kuwainua wakulima ambayo ni kuanzisha vikundi vya kuweka akiba ili kurahisisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo kupitia vikundi hivyo.

Katika taarifa ya kikundi cha Tujikwamue ambayo imesomwa na katibu wa kikundi Bw. Phabian Malikioli amesema kikundi hicho kimeshinda shindano na kupata mashine mbili za kupandia mahindi na maharage na mashine moja ya kupukuchua mahindi.

Malikioli amesema, katika mradi huo wamepata mashamba darasa mawili ya mahindi na maharage yenye ukubwa wa ekali 2 ambazo huwasaidia katika uzalishaji wa mazao yenye ubora.

Mgeni rasmi kwa niaba ya Diwani wa kata ya Mabamba, Afisa Mtendaji Bw. Paskali Ngendabanka amesema wataendelea kuhakikisha vikundi vinapata elimu juu ya kilimo bora.

Naye Afisa Maendeleo halmashauri ya wilaya ya Kibondo Bi. Anastasia Peter amesema halmashauri itaendelea kuvikopesha vikundi ambavyo vinaonyesha nia ya kujikwamua kiuchumi hasa vya wakulima.

Kwa wilaya ya Kibondo mradi wa kilimo tija Kigoma KITIKI kuna vikundi 124 vya wakulima.