Joy FM
Joy FM
5 March 2026, 09:05

Kuwajengea uwezo madiwani kunachangia uongozi bora, uwajibikaji, na utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo, jambo ambalo linaongeza ustawi wa wananchi katika ngazi ya kata na Halmashauri.
Na Mwandishi wetu
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) Sospeter Mtwale amewataka madiwani Nchini kote kusimamia Halmashauri kwa uwazi, weledi na ufanisi katika kuleta Maendeleo ya Wananchi.

Ameyasema hayo alipokuwa akifunga mafunzo elekezi kwa madiwani Kitaifa yaliyofanyikia Manispaa ya Kigoma Ujiji Mkoani Kigoma.
Amewataka madiwani kwa kushirikiana na wataalamu katika kutatua migogoro ya wananchi, kukuza mapato na kusimamia miradi ya maendeleo kwa fedha kutoka Serikali Kuu na mapato ya ndani.

Aidha amewataka kuwa waadilifu na kutanguliza maslahi ya Wananchi katika Utekelezaji wa Majukumu yao.

Katibu Tawala wa Wilaya Mganwa Nzota akitoa salamu za Mkoa kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa amewataka kuzingatia mafunzo waliyoyapata katika kusimamia Halmashauri kwa kukuza Mapato, utekelezaji wa miradi na kutatua migogoro ya Wananchi.

Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mhe. Mussa Maulidi amekipongeza Chuo cha Serikali za Mitaa kwa namna ambavyo kimetoa mafunzo kwa Halmashauri 184 Nchi kote huku akisema wataendelea kusimamia kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria.
