Joy FM
Joy FM
2 March 2026, 09:39

Zao la korosho ni miongoni mwa mazao muhimu ya biashara na korosho imekuwa nguzo muhimu katika kuinua uchumi wa taifa na kuboresha maisha ya wananchi, hasa wakulima wa vijijini.
Na Mwandishi wetu
Wilaya ya Uvinza imedhamiria kuwakilisha vema Mkoa wa Kigoma kwa kuwa kinara wa kilimo cha zao la Korosho.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mheshimiwa Dinnah Mathamani, kupitia kipindi cha Good Morning Kigoma, kinachorushwa na Radio Joy FM, wakati akizungumzia masuala mbali mbali ya shughuli za maendeleo katika Wilaya ya Uvinza.

Amesema wakulima wilayani Uvinza wameendelea kuhamasika na kilimo cha zao la korosho hasa maeneo ya Nguruka, ambako zao hilo linaonekana kustawi zaidi, kama njia ya kujiongezea kipato chao.
Kwa muda mrefu wakazi wa Wilaya ya Uvinza walitegemea sana kilimo cha tumbaku kama zao kuu la biashara lakini kutokana na mahitaji ya kuongeza kipato katika miaka ya hivi karibuni wameanza kujikita kwenye kilimo cha zao la korosho.
Hatua hiyo ni baada ya Taasisi ya Utafiti NALIENDELI kufanya utafiti na kudhibitisha kuwa zao la Korosho linaweza kulimwa na kustawi vizuri katika wilaya hiyo kutokana na rutuba iliyopo.