Joy FM

Serikali na wadau wapiga hatua kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi

19 February 2026, 16:40

Mkuu wa Wilaya Kigoma Rashid Chuachua akiwa katika uzinduzi wa mradi wa Mjamzito na Mtoto Salama, Picha na Mwandishi wetu

Shirika la Thamini Uhai limezindua mradi wa Mjamzito na Mtoto Salama wenye lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi katika mikoa mitatu ya Kigoma, Katavi na Geita

Na Mwandishi wetu

Serikali kwa kushirikiana na wadau wameendelea kupiga hatua muhimu kuelekea kufikia malengo endelevu ya mwaka 2030 ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kufikia vifo 70 kwa vizazi hai laki moja na vifo vya watoto wachanga kufikia vifo 12 katika vizazi hai elfu moja.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro, aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua kwenye uzinduzi wa mradi wa Mjamzito na Mtoto Salama utakaotekelezwa na Shirika la Thamini Uhai, ukilenga kuchangia katika juhudi za serikali za kupunguza vifo vya uzazi na watoto wachanga.

Viongozi mbalimbali wakiwa katika uzinduzi wa mradi wa Mjamzito na Mtoto Salama Kigoma, Picha na Mwandishi wetu

Amesema hatua hizo ni pamoja na kuboresha na kuimarisha miundombinu pamoja na vifaa tiba kwenye sekta ya afya, na kwamba juhudi zinazofanywa na wadau kama vile Shirika la Thamini Uhai ni muhimu katika kufikia malengo hayo.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro, aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua

Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Joachim Masunga, amesema kupitia mradi wa Mjamzito na Mtoto Salama, utaleta tija kubwa kwenye jitihada za kupambana na vifo vitokanavyo na uzazi.

Sauti ya Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Joachim Masunga

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Thamini Uhai Banzi Msumi, amesema mradi wa Mjamzito na Mtoto Salama ni wa miaka mitano na utatekelezwa katika mikoa mitatu ya Kigoma, Geita na Katavi, unakwenda kuimarisha maeneo muhimu manne ya huduma jumuishi za Mama na Mtoto.

Sauti ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Thamini Uhai Banzi Msumi