Joy FM
Joy FM
19 February 2026, 15:44

Serikali kupitia Wizara ya uchukuzi imesema haitosita kuchukua hatua za kisheria kwa wasimamizi wanaopewa dhamana ya kusimamia miradi ya maendeleo ambao wanashindwa kuendana na kasi ya serikali katika utekelezaji na ukamilishaji wa miradi kwa wakati
Na Tryphone Odace
Naibu Waziri wa uchukuzi Mh. David Kihenzile ameeleza kuridhishwa na ukarabati unaoendelea wa Meli ya MV Liemba unayotajwa kukamilika kwake kutarahisha shughuli za usafirishaji ndani ya ziwa Tanganyika.
Akizungumza mara baada ya ziara ya kutembelea bandari ya Kigoma na kujionea ukarabati wa meli hiyo, Naibu Waziri Kihenzile amesema kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha inarejesha usafiri wa meli ndani ya ziwa Tanganyika na kukuza uchumi wa taifa na wananchi kwa ujumla.
Awali akitoa taarifa ya ukarabati wa MV Liemba, Mhandisi wa ukabati wa meli hiyo Luteni Kanali Elias John amesema ukarabati wa meli hiyo umefikia asilimia 55 na wanategemea kufikia mwezi julai utakuwa umekamilika.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa Kigoma, ambaye ni Katibu tawala Wilaya Kigoma Mganwa Nzota amesema miradi inayotekelezwa na serikali hasa iliyopo chini ya Wizara ya uchukuzi itasaidia kuufungua mkoa wa Kigoma na kukua kiuchumi.
Naye Kaimu Meneja Kampuni za Meli Tanzania tawi la Kigoma Amfrey Daniel amesema kukamilika kwa meli ya MV Liemba kutasaidia mzunguko wa biashara na kuunganisha na mataifa mengine kwa uharaka.