Joy FM
Joy FM
17 February 2026, 10:42

Wabunge mkoani Kigoma wametaka miundombinu mibovu ya barabara kupatiwa ufumbuzi, ili kuondoa adha kwa wajawazito kupoteza maisha wakiwa njiani kufuata huduma maeneo mengine na wananchi kushidwa kusafiri
Na Kadislaus Ezekiel
Changamoto ya ukosefu wa daraja katika Mto Maragalasi Kijiji cha Ilagala Wilayini Uvinza Mkoani Kigoma, pamoja na Ujenzi wa barabra ya Mwandiga mpaka Kagunga Wilaya ya Kigoma, mpakani mwa Burundi, imetakiwa kupatiwa ufumbuzi kwa kujenga miundombinu hiyo, ili kuondoa adha kwa wajawazito kupoteza maisha wakiwa njiani kufuata huduma maeneo mengine na wananchi kushidwa kusafiri.
Licha ya Serikali kuendelea kuchukua hatua kwa kutenga fedha za utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, Mkoa wa Kigoma bado unatajwa kukabiliwa na adha ya kuunganishwa hasa vijiji na Wilaya.

Katika kikao cha bodi ya Barabara Mkoa wa Kigoma, wawakilishi wa wananchi ngazi ya jimbo, akiwemo Nuru Kashakali mbunge wa jimbo la Kigoma Kusini, anasisitiza ujenzi wa daraja eneo la mto Maragalasi kijiji cha Ilagala ili kusaidia wajawazito na wananchi, huku mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini Kizza Mayeye akisisitiza ujenzi wa barabara ya Mwandiga – Kagunga.

Baadhi ya wakuu wa Wilaya akiwemo Mkuu wa Wilaya Uvinza Dinnah Mathamani wameeleza kuwa shughuli za uzalishaji zimekuwa zikikwama kisa wananchi kukosa miundombinu bora ya barabara.

Hata hivyo, taarifa kutoka TARURA na TANROADS zinadai kuwa ufinyu wa bajeti ni moingoni mwa sababu zinazokwamisha utekelezaji wa miradi, licha ya jitihada kufanyika.
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro, ambaye ni Mwenyekiti wa Kikao hicho cha bodi ya barabara amesisitiza miradi ya barabara inayojengwa haina budi kutunzwa ili kusaidia wananchi.
