Joy FM

RC Sirro aongoza kikao cha bodi ya barabara Kigoma

16 February 2026, 16:36

Mkuu wa Mkoa Kigoma akizungumza wakati wa kiako cha bodi ya barabara, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kigoma

Wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA pamoja na Wakala wa barabara Nchini TANROADS Mkoa wametakiwa kuwaelekeza wakandarasi kutochimba vifusi jirani na maeneo ya makazi

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro ameongoza kikao cha bodi ya barabara Mkoa wa Kigoma na  kuagiza kufanyika kwa oparesheni Malum kwa ajili ya kudhibiti wizi na uharibifu wa Alama za barabarani katika maeneo mbalimbali  mkoani hapa. 

Balozi Sirro ametoa maelekezo hayo katika kikao hicho kilichofanyika Februari 16, 2026, ambapo amezitaka Kamati za Usalama kwa kila wilaya kudhibiti wanaofanya uharibifu huo kwa kuwafikisha kwenye vyombo vya Sheria. 

Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Kigoma akiwa kwenye kikao cha bodi ya barabara, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kigoma

Aidha, ameuelekeza uongozi wa TANROADS na TARURA Mkoa wa Kigoma kuendelea kushirikiana na uongozi wa Serikali za vijiji na mitaa katika kutoa Elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza alama za barabarani. 

Katika hatua nyingine balozi Sirro  amewataka wananchi wanaojishighulisha na ufugaji kuzingatia kanuni za matumizi bora ya barabara kwa kuepuka kupitisha mifugo kwenye barabara na  kusababisha uharibifu wa miundombinu hiyo. 

Amesema mamlaka za vijiji zinapaswa kutenga maeneo kwa ajili ya njia zitakazotumika kupitisha mifugo kutoka eneo moja kwenda lingine pamoja na zile zinazotumika kupeleka mifugo malishoni. 

Baadhi ya wajumbe wakiwa katika kikao cha bodi ya barabara, Picha na Ofisi ya mawasiliano

Awali akichangia hoja katika kikao hicho Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini Kiza Mayeye ameuomba uongozi wa TARURA  Mkoa kuimarisha mitaro pembezoni mwa barabara wanazosimamia ili kuzifanya ziwe imara na kutumika kwa muda mrefu. 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua ameshauri uongozi wa TARURA pamoja na TANROADS mkoa kuwaelekeza wakandarasi kutochimba vifusi jirani na maeneo ya makazi, jambo linalohatarisha usalama wa wakazi pamoja na kuchangia uharibifu mkubwa wa mazingira na mwonekano wa mji.

Kamanda wa Polisi Kigoma akiwa anazungumza katika kikao cha bodi ya barabara, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kigoma