Joy FM

RC Kigoma akutana na mwakilishi wa ubalozi wa Ufaransa nchini

10 February 2026, 11:39

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amekutana na Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Ufaransa nchini, Jean Traband, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kigoma

Mwakilishi wa ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania amewasili Mkoani Kigoma kwa ajili ya kutembelea kambi za wakimbizi na kukagua miradi inayotekelezwa katika kambi za wakimbizi.

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amekutana na Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Ufaransa nchini, Jean Traband aliyepo mkoani hapa kwa ajili ya ziara ya kutembelea katika Kambi za wakimbizi za Nduta na Nyarugusu ili kujionea hali ya utekelezaji wa miradi na kazi mbalimbali  zinazofanywa na Mashirika na Taasisi zilizo chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR).

Mkuu wa Mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro akiwa kwenye picha na Mwakilishi wa Ubalozi wa Ufaransa nchini na baadhi ya viongozi, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kigoma

Kupitia maongezi ya wawili hao, Balozi Sirro amemueleza mwakilishi huyo kuwa, sambamba na kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya kitaasisi,  atumie fursa hiyo kutazama vivutio vya kiutalii na uwekezaji vilivyopo mkoani Kigoma na kwenda kuvitangaza katika mataifa ya Ulaya ili kuvutia wawekezaji kutoka mataifa hayo kuwekeza mkoani hapa.

Aidha amemueleza mwakilishi huyo kuwa, kwa sasa wakimbizi kutoka nchini Burundi wanaendelea kurejea katika nchi yao pia wale wa kutoka Congo DR, wanaendelea kupatiwa hifadhi huku mipango ya pamoja ya kuwarejesha nchini mwao ikiendelea kufanyika ili hali ya amani itakaporejea waweze kuungana na wenzao katika ujenzi wa taifa lao.