Joy FM
Joy FM
30 January 2026, 18:15

Taka kwa muda mrefu zimekuwa zikichukuliwa kama vitu visivyo na maana na vinavyosababisha uchafuzi wa mazingira, hata hivyo kwa sasa dunia imeanza kubadilisha mtazamo huo kwa kuona taka kama rasilimali muhimu inayoweza kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Na Lucas Hoha
Wanachi Mkoani wa Kigoma wametakiwa kuchangamkia fursa za kiuchumi zinatokana na taka za plastiki, vyuma chakavu na taka za mabaki yatokanayo na zao la mchikichi ili kuinua hali zao kimaisha.

Hayo yamebainishwa na baadhi ya wafanyabiashara wanaotumia fursa za vyuma chakavu na taka za plastiki kwa kuzikusanya taka na kuziuza viwandani kwa kuwezeshwa na shirika la Catholic Relief Service (CRS) wakishirikiana na Shirika la Caritas chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya kupitia mradi wa usimamizi wa taka na usafi wa mazingira (VOICES).
Baadhi ya wafanyabiashra hao akiwemo Idrisa Musa ambaye anakusanya vyuma chakavu katika Kata ya Mwandiga Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wanaeleza namna kazi hiyo ya uchumi rejeshi inavyowasaidia kuondokana na umasikini.

Kwa upande wake, Hassan Kilanoza ambaye ni mmiliki wa kiwanda cha kukamua mafuta ya mawese katika kata ya Simbo anaeleza namna anavyotumia mabaki ya mchikichi baada ya kukamua mafuta kuzalisha mkaa mbadala na kujiingizia kipato.

Simon Mwanjela ni Afisa mradi Mwandamizi kutoka shirika la Catholic Relief Sevirce (CRS) lililopo Manispaa ya Kigoma Ujiji jengo la NSSF anasema vijana wenye mawazo ya ubunifu wa kutumia taka za plastiki kuwa fursa ya kujikwamua kiuchumi watawezeshwa mitaji.
Mradi huo umeanza kutekelezwa tangu mwaka 2024 na utafikia kikomo mwaka 2028 na unatekelezwa katika halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Manispaa ya Kigoma Ujiji na Wilaya Kigoma, ukiwa na lengo la kuwafikia watu zaidi ya laki moja.
