Joy FM
Joy FM
30 January 2026, 08:25

Usalama ni nguzo muhimu katika maendeleo ya taifa lolote kwani bila usalama, shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa haziwezi kufanyika kwa ufanisi na hivyo, mchango wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kigoma wa magari kwa vyombo vya ulinzi na usalama ni hatua muhimu inayostahili kupongezwa.
Na Emmanuel Michael Senny
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikisha upatikanaji wa magari kwa Vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Kigoma ikiwemo Jeshi la Magereza na Jeshi la Zimamoto.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Meneja wa TRA Mkoa wa Kigoma, kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ndugu Yusuph Juma Mwenda, amesema magari yaliyotolewa ni pamoja na gari aina ya Fuso iliyokabidhiwa kwa Jeshi la Magereza na Toyota Alphard iliyokabidhiwa kwa Jeshi la Zimamoto wilaya ya Buhigwe.

Amesema lengo la TRA la kukabidhi magari haya ni kuwasaidia katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kutatua changamoto ya upungufu wa usafiri wa kikazi.
Meneja huyo wa TRA ameongeza kuwa magari hayo yametokana na magari yaliyokamatwa baada ya kuingizwa nchini bila kufuata taratibu za kisheria kwa kutokulipiwa kodi.

Magari hayo yamekabidhiwa kupitia kwa Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dkt. Rashidi Chuachua, na Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina, kabla ya kugawiwa kwa vyombo husika.

Aidha Wakuuu hao wa wilaya wamemshukuru Kamishna Mkuu wa TRA kwa kutambua mchango wa Jeshi la Magereza na Jeshi la Zimamoto na hivyo kuwawezesha kupata magari hayo ambayo yatasaidia sana kuongeza ufanisi wao wa kazi.
Kadhalika wameukumbusha umma wa wananchi kuendelea kutii sheria za kodi na kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiyari kwani kodi ndio msingi wa maendeleo ya nchi huku wakiwasisitiza wananchi na walipakodi kutokujihusisha na biashara za magendo kwani zinapelekea upotevu wa mapato ya serikali.

Kwa upande mwingine, Kamanda wa Jeshi la Magereza wa Mkoa pamoja na Kamanda wa Jeshi la Zimamoto wa Mkoa Kigoma wameishukuru serikali kupitia TRA kwa kuwawezesha kupata magari na kuahidi kuyatunza na kuyatumia katika majukumu yao kama ilivyokusudiwa.