Joy FM
Joy FM
27 January 2026, 15:42

Jamii katika Halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani Kigoma imetakiwa kuwa na desturi ya kupanda miti katika maeneo yanayowazunguka
Na Hagai Ruyagila
Watumishi wa Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma wameadhimisha siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Dkt Samia Suluhu Hassan kwa zoezi la upandaji miti katika Hospitali ya Mji Kasulu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuendelea kutunza na kuboresha mazingira ya hospital hiyo.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu Mwl, Vumilia Simbeye amesema wamemuunga mkono Rais Samia katika siku hiyo kwa kupanda miti hivyo watumishi pamoja na wananchi wote wanatakiwa kuwa wazalendo kwa kufanya hivyo.

Pia amesema kupanda miti kwa wingi ili kuendelea kutunza mazingira ni miongoni mwa mikakati muhimu ya halmashauri katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuhakikisha kunakuwepo mazingira bora na salama kwa jamii.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kasulu Mh. Ayubu Ngalaba amewahimiza wananchi na taasisi mbalimbali kuiga mfano huo kwa kupanda na kutunza miti katika maeneo yao, akisisitiza kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mmoja na una mchango mkubwa katika maendeleo endelevu ya jamii.

Afisa Mazingira wa halmashauri hiyo, Bw. Wambura Mniko amesema kuwa miti hiyo aina ya miparachichi iliyopandwa italeta faida mbalimbali ikiwemo kuboresha hali ya hewa, kutunza mazingira ya hospitali, pamoja na kutoa matunda ambayo yatakuwa na manufaa kwa wagonjwa na watumishi wa hospitali hiyo.

Mganga Mfawidhi wa hospitali ya halmashauri ya Mji Kasulu Dkt Japhari Makombe ameishukuru halmashauri kwa kuchagua hospitali hiyo kuwa sehemu ya zoezi hilo muhimu, akisema kuwa miti hiyo itakapokua itasaidia kuboresha mandhari ya hospitali na kutoa hewa safi.
Zoezi hilo linaendana na maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuhimiza utunzaji wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali asili.