Joy FM
Joy FM
26 January 2026, 14:37

Mkuu wa Wilaya Kasulu Mkoani Kigoma amewataka wazazi kuhakikisha usalama wa watoto wakati wa kwenda shuleni hasa wanaovuka mito wakati wa kwenda shule.
Na Hagai Ruyagila
Wazazi na walezi Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma, wametakiwa kuwa waangalifu kwa kuimarisha usalama wa watoto wao wanapokwenda shuleni ili kuwaepusha na hatari za kusombwa na maji wakati huu wa msimu wa mvua.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu, wakati akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake.
Amesema kuwa mvua zinazoendelea kunyesha zimeongeza hatari ya uwepo wa maji mengi katika mito, mabonde na maeneo ya wazi, hali inayoweza kuhatarisha maisha ya watoto endapo wazazi na walezi hawatakuwa makini.
Amesisitiza kuwa wazazi wanapaswa kuwafuatilia watoto wao kwa karibu, kwakuhakikisha wanawasindikiza wanapoelekea shuleni na wakati wa jioni wanaporejea nyumbani, lengo ikiwa ni kuwazuia kucheza karibu na mito au maeneo yenye maji mengi.
Aidha, Kanali Mwakisu amewasihi wazazi na walezi kutodharau kina cha maji akieleza kuwa hata maji yanayoonekana kuwa machache yanaweza kusababisha madhara makubwa.
Baadhi ya wazazi na walezi wilayani Kasulu wamesema wamepokea wito huo na kuahidi kuongeza uangalizi kwa watoto wao, wakieleza kuwa usalama wa watoto ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano kati ya wazazi, jamii na serikali.