Joy FM
Joy FM
21 January 2026, 16:48

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu amewataka watumishi wa Halmashauri hiyo ili kuhakikisha wanasimamia na kushirikiana kikamilifu katika kubuni na kuimarisha vyanzo mbalimbali vya mapato.
Na Hagai Ruyagila
Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma imekisia kukusanya na kutumia zaidi ya shilingi bilioni 44 katika Mwaka wa Fedha 2026/2027, ambapo kati ya fedha hizo, zaidi ya shilingi bilioni 27 zimetengwa kwa ajili ya mishahara ya watumishi.
Akisoma taarifa ya mapendekezo ya mpango wa bajeti ya mapato na matumizi pamoja na miradi ya maendeleo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027, Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Samweli Sendegeya, amesema bajeti hiyo imeongezeka kwa asilimia 11 ukilinganisha na bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026.

Sendegeya amesema ongezeko hilo linatarajiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi katika sekta mbalimbali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu ambaye pia ni Mwenyekiti wa kikao hicho, Kanali Isaac Mwakisu, amewataka wajumbe wa kikao pamoja na watumishi wa serikali kushirikiana kikamilifu kubuni na kuimarisha vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuhakikisha Halmashauri inafikia malengo yake na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Kasulu (DCC) wamepongeza mapendekezo ya bajeti hiyo, huku wakisisitiza umuhimu wa ukusanyaji wa mapato kwa ufanisi na kwa kuzingatia sheria na taratibu, ili kudhibiti uvujaji wa mapato na kuhakikisha malengo ya maendeleo yanafikiwa.
