Joy FM

Wazazi na walezi watakiwa kukuza vipaji vya watoto Kasulu

21 January 2026, 11:22

Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Western Tanganyika Mhashamu Emmanuel Bwatta, Picha na Hagai Ruyagila

Watoto ni rasilimali muhimu katika jamii yoyote kwani wao ndio viongozi na wataalamu wa baadaye na kila mtoto huzaliwa akiwa na vipaji na uwezo wa kipekee, ambavyo huhitaji kutambuliwa na kuendelezwa.

Na Hagai Ruyagila

Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Western Tanganyika Mhashamu Emmanuel Bwatta amewataka wazazi na walezi wilayani Kasulu Mkoani Kigoma kuendelea kukuza vipaji vya watoto wao ili kuwawezesha kufikia ndoto zao na kuchangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Askofu Bwatta ametoa wito huo wakati akizungumza na waumini wa Kanisa hilo katika ibada maalum ya kumsimika msaidizi wa askofu Kanisa kuu Subdean Mch. Canon Laurent Magogwa.

Amesema kuwa watoto wana vipaji vingi vinavyohitaji kutambuliwa mapema na kupewa msukumo sahihi ili viweze kukua na kuwaletea tija, akisisitiza kuwa jukumu hilo kubwa lipo mikononi mwa wazazi na walezi.

Sauti ya Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Western Tanganyika Mhashamu Emmanuel Bwatta

Akizungumza baada ya kusimikwa Subdean ambaye ni msaidizi wa askofu wa kanisa kuu la Mt. Andrea Mch. Canon Laurent Magogwa amemshukuru askofu kwa kumteua katika nafasi hiyo, Pia amesema atashirikiana vyema na askofu wa dayosisi hiyo kwa kusimamia na kuendeleza maendeleo yaliyopo ili dayosisi hiyo iendelee kusonga mbele na kufikia mafanikio.

Sauti ya Subdean ambaye ni msaidizi wa askofu wa kanisa kuu la Mt. Andrea Mch. Canon Laurent Magogwa
Subdean ambaye ni msaidizi wa askofu wa kanisa kuu la Mt. Andrea Mch. Canon Laurent Magogwa, Picha na Hagai Ruyagila

Naye Mkurugenzi wa Kanisa hilo Kanda ya Ziwa Tanganyika Mch. Canon Zebedayo Rugegera akifundisha neno la Mungu amewahimiza viongozi na waumini wa kanisa hilo kuendelea kumtumikia Mungu kwa furaha, uaminifu na kujitoa, akieleza kuwa huduma ya kweli huambatana na upendo.

Sauti ya Mkurugenzi wa Kanisa hilo Kanda ya Ziwa Tanganyika Mch. Canon Zebedayo Rugegera

Akiwa amemuwakilisha mkuu wa mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro, Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu akitoa salamu za Serikali katika ibada hiyo amesema kanisa hilo limekuwa chachu ya kuhamasisha amani hivyo amewasisitiza waumini hao kuendelea kudumisha amani na usalama katika maeneo yao ili jamii iweze kuendelea na shughuli za uzalishaji.

Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu, Picha na Hagai Ruyagila
Sauti ya Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu

Baada ya kusimikwa, Mchungaji, Canon Laurent Magogwa anakuwa Subdean wa 11 wa kanisa kuu la Mt. Andrea, Katika wadhifa huo, anakuwa msaidizi wa askofu katika kanisa kuu la Mt. Andrea lililopo Mjini Kasulu.

Waumini wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Western Tanganyika, Picha na Hagai Ruyagila