Joy FM

Mkandarasi atakiwa kukamilisha mradi wa maji kwa wakati Kasulu

19 January 2026, 14:47

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Kundo Mathew, akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maji Kasulu, Picha na Hagai Ruyagila

Naibu Waziri wa maji Mhandisi Kundo Matthew amempa siku 60  mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa mradi wa maji wa miji 28 katika Halmashauri ya mji Kasulu Mkoani Kigoma kukamilisha mradi huo.

Na Hagai Ruyagila

Naibu Waziri wa Maji, Mheshimiwa Kundo Mathew, amemuagiza mkandarasi Megha Engineering anayetekeleza mradi wa maji wa Miji 28 katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu kuhakikisha mradi huo unakamilika na kukabidhiwa kwa Serikali ifikapo Julai 22, 2026.

Naibu waziri Mathew ametoa maagizo hayo mnamo januari 18, 2026, wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo wenye thamani ya Shilingi Bilioni 35, ambao awali ulipangwa kukamilika Oktoba 10, 2025.

Naibu Waziri wa Maji, Mheshimiwa Kundo Mathew, akiwa katika ziara ya kukagua mradi wa maji Kasulu, Picha na Hagai Ruyagila

Amesema kunatokana na changamoto zilizojitokeza mradi huo umeshindwa kukamilika kwa wakati hali iliyosababisha kufikia asilimia 57 tu ya utekelezaji hadi sasa. Kutokana na hali hiyo, amesisitiza mkandarasi kuongeza kasi ya kazi ili kuukabidhi serikalini ifikapo julai 22,2026.

Sauti ya Naibu Waziri wa Maji, Mheshimiwa Kundo Mathew

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu, amesema ofisi yake itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu

Awali Mkurugenzi wa mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira  wilaya ya Kasulu (KUWASA) Injinia Hussein Nyemba  akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo amesema mradi huo umeshindwa kukamilika kwa wakati kutokana na sababu mbalimbali zinazowakabili wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

Sauti ya Mkurugenzi wa mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira  wilaya ya Kasulu (KUWASA) Injinia Hussein Nyemba

Mradi wa maji wa Miji 28 unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wananchi laki moja kutoka kata 12 za Halmashauri ya Mji wa Kasulu mkoani Kigoma. Kukamilika kwake kutasaidia kuondoa adha ya upatikanaji wa maji safi na salama, hususan tatizo la maji yenye rangi ambayo kwa muda mrefu yamekuwa changamoto kwa wakazi wa halmashauri hiyo.