Joy FM

COPRA yakabidhi mbegu za mbaazi kwa wakulima Uvinza

14 January 2026, 10:55

Mkuu wa Wilaya Uvinza akipokea mbegu za mbaazi zitakazogawwiwa kwa wakulima, Picha na Ofisi ya mawasiliano Uvinza

Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mh. Dinah Mathamani amesema kuwa kilimo bado ni uti wa mgongo wa uchumi wa wananchi wa Uvinza na kuwa mbegu bora zinasaidia kuongeza mavuno

Na Mwandishi wetu

Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imekabidhi rasmi mbegu za mbaazi kwa wakulima wa Wilaya ya Uvinza kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa zao hilo, kuimarisha usalama wa chakula na kuinua kipato cha wananchi.

Makabidhiano hayo yamefanyika mbele ya viongozi mbalimbali wa wilaya akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mh. Dinah Mathamani, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Mh Salvatory Motto pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Ndg. Kechegwa Masumbuko ambapo wote kwa pamoja wamepongeza jitihada za Shirika la COPRA katika kuunga mkono sekta ya kilimo.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mh. Dinah Mathamani amesema kuwa kilimo bado ni uti wa mgongo wa uchumi wa wananchi wa Uvinza, hivyo upatikanaji wa mbegu bora za mbaazi utasaidia kuongeza mavuno na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wakulima. Ameongeza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo kwa wakati.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Mh. Salvatory Motto amewataka wakulima kutumia mbegu hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuzingatia ushauri wa wataalam wa kilimo ili kupata matokeo chanya.

 Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Kechegwa Masumbuko amesisitiza kuwa halmashauri itaendelea kutoa usimamizi na elimu kwa wakulima ili kuhakikisha mbegu hizo zinaleta tija iliyokusudiwa.

Mkuu wa Kanda ya Magharibi wa COPRA  Liaison Nzunda amesema kuwa shirika hilo limejipanga kuendelea kushirikiana na serikali na wakulima kwa kutoa mbegu bora na msaada wa kitaalamu ili kuchangia maendeleo ya kilimo endelevu.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima walionufaika na zoezi hilo Juma Pilipili kutoka kata ya Basanza ameeleza shukrani zao kwa serikali na COPRA wakisema msaada huo utawasaidia kuongeza uzalishaji wa mbaazi na kuboresha maisha yao.