Joy FM
Joy FM
9 January 2026, 08:54

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeshusha boti ya uokoaji katika Ziwa Tanganyika yenye vifaa vya kisasa ambavyo vitawawezesha kutambua eneo ilipotokea changamoto majini na kufikisha huduma za dharura.
Na Mwandishi wetu
Wasafirishaji wa vyombo vidogo vya majini na upakiaji wa mizigo katika mwalo wa Kigodeko, Ziwa Tanganyika, wamesema kupatikana kwa boti ya uokozi na utafutaji ndani ya ziwa hilo kutawawezesha kunusuru maisha ya abiria na mabaharia pindi ajali zitakapotokea majini.
Wasafirishaji hao wamebainisha hayo baada ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kufanya majaribio ya boti ya pili ya uokozi katika ziwa hilo mkoani Kigoma, hatua iliyorejesha matumaini kwa watumiaji wa vyombo hivyo vya majini.
“Ujio wa boti ya utafutaji na uokozi kwenye ziwa hili umeleta matumaini mapya kwa wasafirishaji wa abiria na mizigo, maana ziwa hili ni kubwa na mara nyingi ajali zinapotokea tunapitia wakati mgumu kupata chombo cha uokozi. Lakini sasa kimepatikana, tuna furaha kubwa sana,” amesema Saidi Muhomi, msafirishaji.
Naye Afisa Mfawidhi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Mkoa wa Kigoma, Adam Mamiro, amesema boti hiyo itakuwa msaada mkubwa siyo tu kwa wakazi wa Kigoma, bali pia kwa mikoa jirani ya Rukwa na Katavi.
Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi Ukaguzi na Usajili TASAC, Grayson Marwa, amebainisha kuwa boti hiyo ina vifaa vya kisasa ambavyo vitawawezesha kutambua eneo lenye changamoto majini na kufikisha huduma za dharura kwa wakati.
TASAC II ni boti ya pili ya uokozi kufanyiwa majaribio ndani ya Ziwa Tanganyika, baada ya boti nyingine kama hiyo kufanyiwa majaribio katika Bandari ya Tanga.