Joy FM
Joy FM
8 January 2026, 08:41

Mkuu wa Wilaya Kasulu Kanali Isack Mwakisu ameielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kuhakikisha ndani ya kipindi cha siku 14 inaandaa maandiko yatakayobainisha matumizi ya majengo ya IRC
Na Mwandishi wetu
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma imekabidhiwa rasmi majengo yaliyokuwa yakitumiwa na Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji (IRC), yaliyopo Kata ya Makere katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, kwa lengo la kuyatumia kwa shughuli za Serikali na maendeleo ya wananchi.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo Januari 7, 2026 ambapo Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mhe. Kanali Isaack Mwakisu, ameyapokea majengo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe.Balozi Simon Sirro.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Kanali Mwakisu amesema majengo hayo yako katika hali nzuri na yanaweza kutumika kwa muda mrefu endapo yatatunzwa ipasavyo.

Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ulinzi wa majengo hayo kwa kushirikiana na jamii inayoyazunguka ili kulinda miundombinu hiyo ya umma.
Aidha, ameielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kuhakikisha ndani ya kipindi cha siku 14 inaandaa maandiko yatakayobainisha matumizi ya majengo hayo pamoja na namna ambavyo wananchi wa maeneo ya jirani ni namna gani watanufaika na uwepo wa miundombinu hiyo.
Awali, Mkuu wa Shirika la IRC Mkoa wa Kigoma, John Misinzo, ameishukuru Serikali kwa kuwapokea tangu walipoingia nchini, jambo lililowawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika Kambi ya Wakimbizi Nyarugusu na kwa jamii wenyeji, zilizofaidika na huduma zao hadi walipohitimisha shughuli zao wilayani humo.

Mbali na Mkuu wa Wilaya, makabidhiano hayo pia yaliwashuhudia Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Theresia Mtewele, Kamati ya Ulinzi ya Wilaya, wakuu wa divisheni na vitengo vya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, watendaji wa kata na vijiji,viongozi wa dini, pamoja na wawakilishi kutoka Shirika la IRC.
