Joy FM
Joy FM
7 January 2026, 08:59

Serikali inaendelea kuchukua hatua katika kuboresha utendaji kazi wa Jeshi la Polisi kwa kuongeza kiasi kikubwa nyenzo za usafiri ili kurahisisha ufikiwaji wananchi na kutatua changamoto zao za kiusalama
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amesema hali ya usalama mkoani hapa imeendelea kuimarika pamoja na uwepo wa changamoto ya idadi kubwa ya wahamiaji haramu kutoka nchi zinazopakana na mkoa, wanaolenga kuingia nchini kujitafutia kipato sambamba na ukosefu wa hali ya amani na utulivu maeneo wanayotoka.

Sirro ametoa kauli hiyo alipokutana Kamishna wa Polisi Jamii CP. Faustine Shilogile akiwa mkoani hapa kwa ajili ya kuendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa wa Polisi Jamii Kanda Namba tano inayohusisha mikoa ya Kigoma, Kagera na Tabora.
Balozi Sirro ameuomba uongozi wa Serikali kupitia jeshi hilo kuendelea kuongeza watendaji katika mkoa, kutokana na uhitaji mkubwa uliopo.

Kwa upande wake, Kamishna Shilogile amesema serikali inaendelea kuchukua hatua katika kuboresha utendaji kazi wa Jeshi hilo ikiwemo kuongeza kwa kiasi kikubwa nyenzo za usafiri ili kurahisisha ufikiwaji wananchi na kutatua changamoto zao za kiusalama.