Joy FM
Joy FM
31 December 2025, 12:38

Na Esperance Ramadhan
Katika kuendelea kuhakikisha jamii inakuwa na afya njema, Jamii imetakiwa kutekeleza afua za lishe kwa kutoa elimu ya afya na lishe kwa wazazi na walezi.
Lishe bora ni msingi mzuri wa afya bora na inachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya ukuaji wa kimwili na kiakili kwa mtoto.
Kwa kutambua ukubwa na umuhimu wa kuondokana na udumavu kwa watoto Afisa mtendaji wa mtaa wa rutale kata ya kipampa Bw Mathayo Edward amesema tangu kuanzishwa kwa siku ya afya na lishe ya kijiji (SALIKI) imesaidia kuwapa elimu wazazi na walezi namna ya kuandaa lishe bora na kupunguza hali ya udumavu wa watoto.
Aidha amewataka wazazi na walezi kujitokeza katika siku ya afya na lishe ya kijiji SALIKI ili kuendelea kupata elimu ya uandaaji mzuri wa chakula cha watoto kwa kuzingatia makundi sita ya chakula.
Kwa upande wao, Baadhi ya wazazi waliyopatiwa elimu wamesema wataitumia katika familia zao na kuhamasisha jamii inayowazunguka kwa kuwapa elimu waliyoipata wao.
Takwimu za 2023 zinaonyesha mkoa wa Kigoma ulifanya vizuri katika kupambana na utapiamlo ingawa changamoto ya kutokula mlo kamili bado ipo na inahitaji juhudi zaidi katika kuhamasisha lishe bora.