Joy FM
Joy FM
26 December 2025, 12:52

Halmashauri ya Wilaya Kibondo Mkoani Kigoma imesema kuwa utekelezaji wa afua za lishe umesaidia kuongeza ufaulu chanya kwa wanafinzi shuleni
Na Mwabdishi wetu
Kikao cha tathmini ya utekelezaji wa afua za lishe kwa robo ya kwanza ya mwaka, kwa kipindi cha Julai hadi Septemba, kimefanyika 23 Desemba 2025 katika ngazi ya wilaya, kikihusisha wajumbe wa Kamati ya Lishe ya Wilaya.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Katibu Tawala wa Wilaya, Upendo Malango, amewahimiza Watendaji wa Kata kuendelea kuwahamasisha wazazi na walezi kuchangia chakula mashuleni, akisisitiza kuwa lishe bora ni nguzo muhimu katika kuboresha elimu na afya ya watoto.

Amesema upatikanaji wa chakula shuleni huchangia kuongeza mahudhurio, umakini darasani na ufaulu wa wanafunzi.
Aidha, Katibu Tawala wa Wilaya Kibondo amewataka Watendaji wa Kata kwa kushirikiana na uongozi wa shule kuhakikisha shule zinatenga maeneo maalum kwa ajili ya mashamba ya shule ili kulima mazao ya chakula.
Hatua hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa chakula shuleni na kuimarisha lishe kwa wanafunzi kwa njia endelevu.
Kwa upande wake, Afisa Lishe wa Wilaya Kibondo Tumaini Muna, amesema utekelezaji wa afua za lishe bora umeleta matokeo chanya ikiwemo kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi shuleni, hali inayochangiwa na wanafunzi kupata chakula chenye virutubisho stahiki.
Kikao hicho kililenga kutathmini utekelezaji wa afua za lishe katika robo ya kwanza pamoja na kuweka mikakati ya kuimarisha lishe kwa watoto, hususan wale waliopo katika umri wa shule, ili kuhakikisha wanapata mazingira bora ya kujifunza na kukua kiafya.