Joy FM
Joy FM
10 December 2025, 15:24

Na Daniel Amando
Jumuiya ya Watu Wenye Kuhuisha Tabia za Kiislam Tanzania JAI, Mkoa wa Kigoma, imepiga hatua muhimu katika kutoa huduma za kiutu kwa wagonjwa, baada ya kupatiwa msaada wa gari la wagonjwa kutoka kwa wadau wa huduma za kijamii.
JAI Kigoma imejikita katika kujitolea kutoa huduma za kiutu hususani kwenye sekta ya afya ambapo hutoa huduma ya chakula, kulipia matibabu na usafiri kwa wagonjwa wenye rufaa wasiojiweza, lakini ukosefu wa gari la wagonjwa ulikuwa ukitatiza huduma hizo.
Akiongea baada ya JAI kukabidhiwa gari la wagonjwa lenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 200 kutoka Taasisi ya The Islamic Foundation, Katibati wa JAI Mkoa wa Kigoma Siasa Juma Barakabitse, amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuleta ustawi wa jamii wanayoihudumia.
Hafla ya kukabidhi gari hilo imeshuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua, ambaye amezindua rasmi huduma za gari hilo kisha kutoa neno la kupongeza mchango wa JAI katika jamii ya Kigoma.
Mkurugenzi wa Taasisi ya The Islamic Foundation, Mkoa wa Kigoma Mensh Omary Senga, amesema gari hilo ni utekelezaji wa ahadi ya Mwenyekiti wa taasisi hiyo aliyoitoa kwa JAI takribani wiki mbili zilizopita, kufuatia ombi lao wakati alipotembelea Hospitali ya Maweni ambapo JAI hufanya kazi zake za kuhudumia wenye uhitaji.