Joy FM
Joy FM
10 December 2025, 14:13

Wakati madiwani wa Halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Kigoma wakiwa wameshakula kiapo cha kuanza kuwatumikia wananchi kwa kipindi cha miaka mitano msisitizo upo kwenye ukusanyaji wa mapato ili yaweze kusaidia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali
Na Hagai Ruyagila
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Elisante Mbilo, amewataka Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato ili kuiwezesha halmashauri hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza na Madiwani pamoja na watumishi wa serikali wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Mbilo amewataka viongozi hao kutekeleza wajibu wao kikamilifu na kusimamia ipasavyo ukusanyaji wa mapato ya ndani, akibainisha kuwa hatua hiyo itasaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kasulu, Mbelwa Chidebwe, amewahimiza madiwani kuungana na kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha mapato ya halmashauri yanakusanywa kwa ufanisi ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya mji.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini, Profesa Joyce Ndalichako, amesema wananchi wana matarajio makubwa kwa viongozi waliowachagua, hivyo ni muhimu kuwa karibu nao na kusikiliza changamoto zinazowakabili ili kuchukua hatua stahiki.
Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu wametoa ahadi ya kusimamia kwa umakini vyanzo vyote vya mapato kwa kushirikiana na wananchi, ili kuongeza mapato yatakayowezesha halmashauri kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.