Joy FM
Joy FM
8 December 2025, 09:06

Vyombo vya ukamataji na upelelezi mkoani Kigoma, vimetakiwa kutotumia vibaya madaraka badala yake vifuate kanuni za ukamataji na kuhakikisha kwamba suala la upelelezi na uchunguzi wa mashauri linafanyika kwa uadilifu weledi na uwajibikaji wa hali ya juu ili kuepuka kuharibu kesi, kusababisha kero kwa watu kwa kutotenda haki.
Na Hagai Ruyagila
Watumishi wa taasisi za NPS, TAKUKURU, Jeshi la Polisi na Uhamiaji Mkoani Kigoma wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na kufuata sheria ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa wakati na kuzingatia huduma bora za mashitaka na usawa kwa wote.
Hayo yamejiri wakati wa kuhitimisha mafunzo ya Siku mbili ambayo yamezikutanisha taasisi za watumishi wa NPS,TAKUKURU,jeshi la Polisi na idara ya uhamiaji mafunzo ambayo yamefanyika mjini Kasulu ambapo mada 9 zimetolewa kwa Watumishi hao.
Mkuu wa mashitaka Mkoa Wa Kigoma Waziri Magumbo Anaeleza dhima ya mafunzo hayo katika kuhakikisha wanapunguza mrundikano wa mashauri Mahakamani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kigoma Alfred Kasoro amewataka watumishi hao kuyatumia mafunzo waliyopatiwa kuleta ufanisi kwa wananchi kwa kutenda haki.
Afisa uhamiaji Mkoa wa Kigoma kamishina msaidizi mwandamizi Dismas Mulura amehimiza kufanya kazi kwa ushirikiano.
Akifunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya Ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu, Katibu tawala wilaya ya Kasulu Bi.Theresia Mtewele ametoa wito wa kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
