Joy FM
Joy FM
5 December 2025, 13:44

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania amehimiza watendaji wa vyombo vinavyohusika na ukamataji na upelelezi kufuata taratibu na sheria
Na Emmanuel Matinde
Vyombo vya ukamataji na upelelezi mkoani Kigoma, vimetakiwa kutotumia vibaya madaraka badala yake vifuate kanuni za ukamataji na kuhakikisha kwamba suala la upelelezi na uchunguzi wa mashauri linafanyika kwa uadilifu weledi na uwajibikaji wa hali ya juu ili kuepuka kuharibu kesi, kusababisha kero kwa watu kwa kutotenda haki.
Kauli hiyo imetolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Augustino Rwizile, wakati akifungua mafunzo ya weledi kwa wapelelezi na waendesha mashtaka wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka NPS Mkoa wa Kigoma, yaliyojumuisha pia TAKUKURU na Uhamiaji.

Mafunzo hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Ofisi za Halmashauri ya Mji Kasulu, yakilenga kujengeana uwezo wa upelelezi wa makosa ya jinai na kuendesha mashtaka, kubadilishana uzoefu wa kiutendaji katika masuala ya upelelezi pamoja na uendeshaji wa mashtaka.
Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kigoma Alfred Kasoro, na Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Kigoma Waziri Magumbo, wameeleza katika mafunzo hayo namna wanavyoumizwa na suala la baadhi ya wapelelezi na wachunguzi kukosa weledi na kusababisha kukwama mahakamani.
Awali Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini TAKUKURU Mkoa wa Kigoma, Asha Kwariko, amesema kwa pamoja wamejipanga kuhakikisha mlolongo wa haki jinai unatekelezwa kwa ufanisi katika mkoa wa Kigoma.