Joy FM
Joy FM
4 December 2025, 14:17

Chakula ni sehemu muhimu sana katika maisha ya mwanafunzi shuleni hasa walio katika umri wa ukuaji, wanahitaji virutubisho vya kutosha kama protini, vitamini, madini, na wanga ili miili yao ikue kwa afya lishe duni inaweza kusababisha kudumaa, udhaifu, na magonjwa ya mara kwa mara.
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe. Dkt. Rashid Chuachua, ametoa wito kwa shule zote ndani ya Wilaya kuendeleza na kuongeza jitihada za kilimo cha mazao ya chakula shuleni, hatua itakayowezesha Wanafunzi kupata chakula cha uhakika na kuboresha mazingira yao ya kujifunzia.
Akizungumza leo tarehe 4 Desemba 2025, katika Kikao cha tathmini ya Mkataba wa Lishe kilicholenga kujadili utekelezaji wa Afua za Lishe kwa Robo ya Kwanza (Julai–Septemba), Dkt. Chuachua amesema kuwa kilimo mashuleni ni sehemu muhimu ya kuongeza upatikanaji wa chakula, kupunguza changamoto za utoro na kuinua ufaulu.

Amesisitiza kuwa Wanafunzi wanapaswa kushiriki kikamilifu Shughuli za kilimo hususan kwenye shule zenye mashamba yanayozalisha mazao kama mahindi, maharage, mboga mboga na viazi, hivyo kujenga utamaduni wa kujitegemea na kuchangia katika mapambano dhidi ya udumavu kwa watoto.
Dkt. Chuachua ameziagiza kamati za shule, walimu na viongozi wa jamii kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kupanga, kusimamia na kutathmini utekelezaji wa shughuli za lishe ili kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya kujifunza katika mazingira mazuri na salama.
