Joy FM
Joy FM
4 December 2025, 12:13

Kituo cha afya cha Mwamintare kilichopo Halmashauri ya Mji wa Kasulu kinahudumia kata tatu ya Muhunga, Mganza na Heru Juu kwa wakazi 50887.
Na Hagai Ruyagila
Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini mkoani Kigoma Profesa Joyce Ndalichako amekabidhi gari la kubebea wagonjwa katika kituo cha Afya cha Mwamintare kilichopo kata ya Heru Juu Halmashauri ya Mji Kasulu ili kuwasaidia kuimarisha utoaji wa huduma za dharura kwa wananchi wa eneo hilo.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano Profesa Ndalichako amesema kukabidhi gari hilo ni sehemu ya jitihada ya kuboresha sekta ya afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa haraka na usalama wanapopata dharura.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Kasulu Mwl. Vumilia Simbeye ameishukuru serikali kupitia mbunge huyo kwa msaada huo akibainisha kuwa gari hilo litapunguza changamoto ya usafiri wa wagonjwa na kuongeza ufanisi wa huduma bora za afya katika eneo hilo.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya Mji Kasulu Mh. Ayubu Ngalaba, amewataka watumishi wa kituo gicho pamoja na wananchi kulitunza gari hilo na kuhakikisha linatumika kwa kazi iliyokusudiwa ili liendelee kutoa manufaa kwa muda mrefu.
Awali, akisoma taarifa ya kituo hicho, Mganga mfawidhi wa kituo cha afya cha Mwamintare Dr. Mgoba John amesema upatikanaji wa gari hilo utasaidia kusafirisha wagonjwa kwa haraka hali ambayo itasaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na vifo vya watoto.