Joy FM
Joy FM
3 December 2025, 11:22

Katibu tawala wa Wilaya Kasulu Mkoani Kigoma Bi. Theresia Mtewele amewataka madiwani kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi
Na Hagai Ruyagila
Diwani wa Kata ya Kigondo, Ayubu Ngalaba (CCM), amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kasulu baada ya kupata kura 19 kati ya kura 22 zilizopigwa na Madiwani wa halmashauri hiyo.
Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi huo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Bi. Theresia Mtelewe, amesema jumla ya kura zilizopigwa ni 22 ambapo diwani wa kata ya Kigondo Ayubu Ngalaba CCM amepata kura 19, huku Diwani wa Kata ya Msambala, Daniel Digimbi (ACT-Wazalendo), akipata kura 3.

Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Diwani wa Kata ya Kumsenga, Hosea Nkayamba (CCM), amechaguliwa kwa kura zote 22 za wajumbe, akimshinda Diwani wa Kata ya Heru Juu, Gilbert Isambe (ACT-Wazalendo), ambaye hakupata kura yoyote.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mh. Ayubu Ngalaba, aliwashukuru madiwani wote waliomchagua na kuahidi kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi ya utawala bora bila upendeleo.

Huu ni mkutano wa kwanza wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji Kasulu, ambapo pamoja na uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti, madiwani wamepata fursa ya kuunda kamati mbalimbali za halmashauri zitakazosaidia kusukuma mbele maendeleo ya mji huo.