Joy FM

Watumishi wa umma watakiwa kutumia PSSSF kidijitali Kigoma

26 November 2025, 12:59

Muonekano wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Picha na Mtandao

Watumishi wa Mkoani Kigoma wamepongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kuboresha huduma zake za kuanza kutoa huduma kidijitali

Na Emmanuel Matinde

Maafisa Utumishi na Wahasibu kutoka taasisi mbalimbali za Serikali wametakiwa kutumia mifumo ya kidigitali inayotolewa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ili kurahisisha ulipaji wa michango na uwasilishaji sahihi wa taarifa za wanachama kwa wakati.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma katika semina kwa waajiri wa mkoa wa Kigoma, kwa maafisa wanaoshughulikia masuala ya wananchama wa PSSSF, Afisa Manunuzi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Patrick Kigere, amesema kuwa matumizi sahihi ya mifumo ya kisasa ya PSSSF ni hatua muhimu katika kuhakikisha wanachama wanapata mafao yao kwa wakati kwa mujibu wa sheria.

Aidha, amesisitiza kwa waajiri wote kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi, uadilifu na umakini ili taarifa za wanachama ziwasilishwe kikamilifu kwenye mfumo wa PSSSF.

Sauti ya Afisa Manunuzi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Patrick Kigere

Kwa upande wake, Meneja wa PSSSF Kanda ya Ziwa Magharibi Thomas Rabi, amesema semina hiyo imelenga kuongeza uelewa kwa waajiri kuhusu matumizi ya mifumo ya kidigitali ili kuwawezesha waajiri kutoa taarifa kwa haraka, kufuatilia michango, pamoja na kuzuia changamoto za ucheleweshaji ambazo zimekuwa zikijitokeza.

Sauti ya Meneja wa PSSSF Kanda ya Ziwa Magharibi Thomas Rabi

Nao maafisa utumishi na wahasibu waliohudhuria semina hiyo akiwemo Farida Amani na Anzuruni Kasule wamesema mafunzo waliyopata yatawasaidia kuboresha usimamizi wa taarifa za watumishi, kupunguza makosa ya uwasilishaji na kuongeza uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao.

Sauti ya maafisa utumishi na wahasibu waliohudhuria semina hiyo