Joy FM
Joy FM
25 November 2025, 12:34

Wavuvi katika Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma wamelalamikia matukio ya kuvamiwa na kuporwa zana za uvuvi ambapo wameiomba Serikali kuchukua hatua ili kudhibiti uhalifu na wahalifu wanaofanya matukio hayo ya wizi kwa wavuvi wakiwa katika majukumu yao nyakati za usiku.
Na Kadislaus Ezekiel
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amekutana na kuzungumza na wavuvi pamoja na wachakataji wa mazao ya uvuvi juu ya kero ya ujambazi wanaofanyiwa uvuvi katika Ziwa Tanganyika na kuporwa zana zao za uvuvi na hata maisha yao kuwa hatarini.
Wakizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa Balozi Simon Sirro, katika eneo la mwalo wa Katonga Manispaa ya Kigoma Ujiji, baadhi ya wavuvi na wachakataji wa mazao ya uvuvi kama ambavyo siku zote kimekuwa kilio chao, wametaka wavuvi kuthaminiwa na kupatiwa ulinzi wa kutosha.
Akijibu maombi ya wavuvi na wachakataji wa mazao ya uvuvi, Balozi Sirro, amewahakikishia kuwa itafanyika misako na doria za kudhibiti ujambazi ambao umepelekea pia wavuvi kupoteza maisha karibu kila mwaka.
Hivi karibuni Jeshi la Polisi mkoani Kigoma limepokea boti ya mwendokasi yenye thamani ya Shilingi Milioni 400 kutoka makao makuu kwa ajili ya doria ya kudhibiti uhalifu na kuimarisha usalama kwa wavuvi katika Ziwa Tanganyika.